Na Mwandishi wetu,
Morogoro.
HALMASHAURI za wilaya hapa nchini, zimetakiwa kuongeza
ufanisi katika kusimamia miradi ya maji kwa kuchangamkia fursa ya fedha za
kitanzania bilioni 250 zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Uingereza (DFID) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji safi na
salama vijijini kwa mwaka 2016-2020.
Mkurugenzi msaidizi wa Wizara ya maji na umwagiliaji Injinia
Jackson Mutazamba aliwaambia wakurugenzi wa wilaya katika semina inayofanyika
mjini Morogoro jana kuwa ni halmashauri chache tu ndio zimeanza kupata fedha
hizi mara baada ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa na wafadhili hao.
“Kuna fedha za kutosha katika mradi huu ukilinganisha na
mwamko wa halmashauri katika kuchangamkia fursa hii ya kuongeza mtandao wa maji
katika maeneo yao”, alisema na kuongeza kuwa fedha hizi zinaweza kuzisaidia
halmashauri kuanzisha miradi mipya na kukarabati ile ya zamani ili iweze kutoa maji
kwa wakati wote wa mwaka.
Alisema moja ya sharti la upatikanaji wa fedha hizi ni
ufanisi katika utekelezaji wa miradi iliyopita na ubora wa ripoti za kila mwezi
kama ambavyo programu hii inavyozitaka halmashauri, huku akieleza kuwa kigezo
hiki ni muhimu katika kuvuka hatua moja hadi nyingine na kupata fungu kubwa zaidi
la fedha ambalo litawezesha kutekeleza miradi mikubwa zaidi katika halmashauri
husika.
Kwa mfano halmashauri zinaweza kupokea aina mbili za malipo
kama vile paundi za kiingereza 50 kwa ajili ya kuendeleza kituo cha maji na
fungu hili linaweza kuongezeka hadi paundi 1,500 kulingana na ufanisi wa utekelezaji
katika hatua ya mwanzo.
“Ukipata paundi zaidi ya 1,500 kwa mara moja kwa miradi ya
vijijini ni nyingi sana katika kuiboresha na kuifanyia matengenezo ya mara kwa
mara ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wote, pia fedha hizi zinaweza
kutumika kuanzisha vituo vipya vya kusambazia maji hivyo kufanya mtandao wa
maji kuwa mkubwa zaidi katika eneo husika”, alisema.
Alisema ni halmashauri 57 tu ambazo zimeweza kuvuka vigezo
viwili vya mwanzo kwa mwaka jana na kuweza kupata fungu kubwa zaidi la kiasi
cha paundi za Uingereza 5,000, fedha ambazo kwa miradi ya maji vijijini
zinaweza kusaidia katika upatikanaji wa maji wakati wote wa mwaka.
Aliwahimiza wakurugenzi wa wilaya kuchangamkia fursa hii ya
fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mingi ya maji na kuifufua ile ambayo
imekufa ianze kufanya kazi tena na kuongeza mtandao wa maji kuwa mkubwa zaidi
ili kufikia adhma ya serikali ya asilimia 95 ya watu wanaopata maji katika
miaka michache ijayo.
Injinia Mutazamba aliongeza kwa kusema kuwa lengo la
kuwakutanisha wakurugenzi wote nchini katika semina hiyo ni kuweza kuwaeleza
kwa kina kuhusu fursa hii ya fedha za wafadhili ambazo bado zipo nyingi na
zinaweza kusaidia kupunguza na hata kumaliza kabisa tatizo la maji hasa sehemu
za vijijini.
Alisema programu hii ya kuongeza mtandao wa maji vijijini
unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya shirika la kimataia la DFID la Uingereza
na serikali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment