Rais Dokta John Magufuli. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MRADI wa maji ambao umejengwa katika kitongoji cha Mnazi
mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, umeendelea
kuingia dosari na kuchukua sura mpya baada ya Wananchi wa kata hiyo kuendelea kulalamikia
kwamba mradi huo umekuwa ukitoa maji machafu ambayo hayafai kwa matumizi ya
binadamu.
Kadhalika licha ya kuunyoshea kidole kwamba unadaiwa kujengwa
chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji wananchi katika maeneo husika, bado wakazi hao wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli
kuingilia kati na kuwachukulia hatua kali watendaji wote waliohusika na usimamizi mbovu
juu ya mchakato wa ujenzi wa mradi huo.
Baadhi yao wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa kuomba majina
yao yasitajwe katika mtandao huu walisema kuwa wameshangazwa na serikali kwa kutochukua hatua za
haraka licha ya kulalamikia jambo hilo kwa muda mrefu, hadi ilipofikia hatua ya kiongozi
wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour kutoa agizo lake Mei 8
mwaka huu kwa kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye aunde Kamati ya
kushughulikia suala hilo na kumpatia majibu haraka iwezekanavyo.
Walisema kuwa mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014
kwa gharama ya shilingi milioni 718,896,533 chini ya ufadhili wa benki ya dunia
ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike mapema katika kipindi cha mwaka mmoja
tangu uanze kujengwa, lakini inashangaza kuona kwamba hadi kufikia kipindi cha
mwaka huu 2017 ujenzi huo bado haujakamilika na sehemu kubwa ya fedha za mradi
huo zimekwisha tumika.
“Mradi huu tumekuwa tukiulalamikia siku nyingi miaka mingi iliyopita lakini hakuna hatua zilizokuwa zikichukuliwa, leo mpaka anakuja kiongozi wa mbio
za Mwenge wa Uhuru kutoa amri ya kushughulikia suala hili ndiyo linashughulikiwa, kwa kweli inatuuma
sana”, walisema.
Walidai kuwa wanaimani kwamba matumizi ya fedha hizo katika
mradi huo wa maji zilikuwa zikitumika vibaya, ndiyo maana mradi umejengwa chini
ya kiwango na wananchi wanaendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.
Kufuatia kuwepo kwa sakata hilo Mhandisi wa idara ya
maji katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Vivian Mndolwa ambaye alikuwa
akisimamia ujenzi huo hivi sasa amesimamishwa kazi kwa ajili ya kupisha
uchunguzi juu ya malalamiko hayo na kufuatia pia agizo lililotolewa na kiongozi
huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, baada ya kukataa kuufungua mradi huo alipokuwa
katika kata hiyo ya Mkako wilayani humo.
Kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imetajwa kuwa ni ya
Patty Interplan ya kutoka Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Kaimu Mkurugenzi mtendaji halmashauri
ya wilaya ya Mbinga, Dkt. Patrick Banzi alithibitisha kusimamishwa kazi kwa Mhandisi
huyo na kueleza kuwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo imeunda Kamati maalum ya watu
saba ambao ni wataalamu wanaochunguza tuhuma hizo na mambo mengine
yanayohusiana juu ya mradi huo na taarifa yake itatolewa baadaye mara
itakapokamilisha kazi yake.
No comments:
Post a Comment