Na Mwandishi wetu,
Songea.
KATIKA Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,
imeelezwa kuwa jumla ya vijana 208 wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya
kuanzia kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu.
Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alitoa
takwimu hizo akieleza kuwa katika kundi la waathirika hao Wanawake wapo nane na
wanaume ni 200 ambao wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 45.
Kwa mujibu wa Ofisa habari huyo alifafanua kuwa waliokamatwa
na dawa za kulevya kwa mwaka huu wapo 16 na kwamba baadhi yao mashauri tisa yamefikishwa
Mahakamani huku kesi mbili tayari zimehukumiwa kutokana na matumizi ya madawa
hayo.
Alisema kuwa matumizi ya dawa hizo hasa kwa vijana katika Manispaa
hiyo bado ni tatizo kubwa kama ilivyokuwa nchi nzima na duniani kote kwa
ujumla.
Takwimu zinaonesha kwamba katika kipindi cha mwaka jana Manispaa
ya Songea ilikuwa na waathirika wa dawa za kulevya 97 wakiwemo wanaume 95 na wanawake
wawili.
“Tunatoa wito kwa wananchi wote kutojihusisha kwa namna
yeyote ile na matumizi ya dawa hizi za kulevya, halmashauri yetu kwa
kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ambao ni HJFMRI-WRP na Chama cha Uzazi na
Malezi bora (UMATI) kinatoa huduma rafiki kwa makundi haya ili kupunguza hata
maambukizi mapya ya ugonjwa wa Virusi Vya Ukimwi”, alisema.
Jumla ya vituo saba vimekuwa vikitoa huduma ya afya kwa
makundi hayo yaliyopo katika hatari ya kupata VVU ambapo huduma hizo hutolewa
na watoa huduma waliopata mafunzo maalum kulingana na mwongozo wa utoaji wa
huduma husika.
Hata hivyo Midelo alieleza kuwa hadi sasa Manispaa ina jumla
ya wateja 160 waliosajiliwa katika huduma hizo ambapo kati yao wanaume ni 120
na wanawake ni 40 na kwamba wote hao wamepima VVU na kati yao wateja
30 wamegundulika kuwa na maambukizo hayo.
No comments:
Post a Comment