Na Mwandishi wetu,
Songea.
IMEBAINISHWA kuwa ugonjwa hatari wa malaria katika kipindi
cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana, katika Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma umesababisha vifo vya watu 87 sawa na asilimia 10.9 ya vifo vyote 798
vilivyotokea kutokana na magonjwa mengine.
Kwa mujibu wa taarifa iliyomfikia mwandishi wetu kutoka kwa
Afisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa katika vifo hivyo watoto
chini ya miaka mitano waliokufa kutokana na ugonjwa wa malaria walikuwa 34 ambao
ni sawa na asilimia tisa ya vifo vyote vilivyotokea kwa watoto chini ya umri wa
miaka mitano ambavyo vilikuwa 401.
Midelo alisema kuwa mwaka 2016 Manispaa ya Songea ilikuwa na
wagonjwa wa malaria waliopata matibabu ya nje 5,928 ambao ni sawa na asilimia 2.4
ya wagonjwa wote 244,245 waliopata matibabu ya nje.
Alisema kuwa wagonjwa waliogua ugonjwa wa malaria na kulazwa
kwa mwaka huo ni sawa na asilimia 2.5 ya wagonjwa wote 244,425 waliolazwa.
Pia aliongeza kuwa watoto chini ya umri wa miaka mitano
waliougua ugonjwa wa malaria na kutibiwa kwa matibabu ya nje walikuwa 2,258
sawa na asilimia 3.3 ya wagonjwa wote 68,796 chini ya miaka mitano na wale waliolazwa ni watoto 2,374 sawa na asilimia 3.1 ya
watoto wote waliougua ugonjwa huo.
Katika kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, Manispaa
imejiwekea mikakati ambapo baadhi yake ni kuendelea kushirikiana na serikali katika kuendesha zoezi la mpango
wa ugawaji wa vyandarua shuleni, akina mama wajawazito wakiwemo na watoto
wadogo.
Mikakati mingine ameitaja kuwa ni kuendelea kununua dawa,
vipimo vya kutosha vya (MRDT) na kusambaza kwenye vituo vya kutolea huduma za
Afya, utoaji elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua, kupima kabla ya
kutibiwa, kuwahi matibabu mara unapoona dalili za malaria, kuwahi kliniki na
kuweka mazingira ya kuishi katika hali ya usafi.
Afisa habari huyo alifafanua kuwa Manispaa ya Songea itaendelea
pia kushirikisha wadau mbalimbali katika kudhibiti ugonjwa wa malaria, kutoa
tiba tahadhari kwa akina mama wajazito, kufanya ufuatiliaji, usimamizi na
tathmini ya mwenendo wa ugonjwa wa malaria na kuendelea kuwachukulia hatua za kisheria
wakazi wanaokiuka taratibu, kanuni na sheria za afya na usafi wa mazingira.
Katika hatua nyingine jitihada ya kukabiliana na ugonjwa wa
malaria, Manispaa ya Songea imeanzisha mradi wa kugawa vyandarua bure kwa wazee
1,000 wasiokuwa na uwezo wa kununua vyandarua kutoka katika kata zote 21 zilizopo
mjini hapa.
No comments:
Post a Comment