Hali ya maghuba ya kuhifadhia taka jinsi ilivyo. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amechukizwa na
hali ya mji wa Mbinga mkoani humo kuwa katika hali ya uchafu na kwamba ametoa
agizo kwa viongozi husika wahakikishe kwamba ndani ya wiki mbili, mji huo
unakuwa katika hali ya usafi.
Agizo hilo la Mkuu huyo wa mkoa alilitoa jana wakati
alipokuwa akizungumza na Wazee wa mji wa Mbinga katika kikao maalum
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa, ambacho
kililenga kusikiliza kero zao mbalimbali.
Hoja ya mji huo kuwa mchafu ilianza kuibuliwa na mkazi mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Yordan Konzo na kuungwa mkono na Wazee wenzake,
ambapo walieleza kuwa taka zimekuwa hazizolewi kwa muda mrefu katika maghuba ya
kuhifadhia taka, jambo ambalo limefikia hatua taka hizo zimekuwa zikitoa harufu
na kuwa kero katika makazi ya watu na jamii kwa ujumla.
“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa mji huu ni mchafu unanuka sana,
tumekuwa tukilalamika siku nyingi kwenye mikutano husika lakini hakuna hatua
zinazochukuliwa na mji bado ni mchafu ni vizuri sasa, uwekwe mkakati kabambe wa
kupambana na mazingira haya ili yawekwe katika hali nzuri ya usafi”, alisisitiza
Konzo.
Kwa upande wake Dkt. Mahenge alipomtaka Mkurugenzi mtendaji
wa mji huo, Robert Mageni kutolea ufafanuzi juu ya kero hiyo Mkurugenzi huyo
alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kueleza kuwa, hatua zitachukuliwa za kuusafisha
mji huo ili uweze kuwa katika hali ya usafi.
“Tatizo kubwa linalotukabili hapa Mheshimiwa Mkuu mkoa ni
kutokana na kukosa rasilimali fedha, magari ya kuzolea taka na vifaa kwa ujumla
vya kufanyia kazi hii lakini tumeanza zoezi la uzoaji wa taka hizi kulingana na
vifaa vichache tulivyonavyo kwanza”, alisema Mageni.
Pamoja na Mkurugenzi huyo kutolea maelezo hayo Dkt. Mahenge bado
alieleza kuwa uwezo wa halmashauri hiyo kuzoa taka hizo katika maghuba yaliyopo
mjini humo upo, hivyo wanachopaswa ni kutilia mkazo suala hilo na sio
kulifanyia uzembe kwa kuacha taka zirundikane kwa muda mrefu kwenye maghuba
hayo.
Aliongeza kuwa mji wa Mbinga hautakiwi kuwa katika hali ya
uchafu lengo la kufanya hivyo ni kuweza kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama
vile kipindupindu na kwamba, amewataka viongozi wanaosimamia masuala ya usafi
washirikishe jamii katika maeneo yao wanayoishi ili waweze kuchangia kidogo
gharama za uzoaji taka na usafi kwa ujumla ndani ya mji huo.
“Baada ya wiki hizi mbili kupita nitakuja mwenyewe kukagua
mji huu kama agizo langu la usafi wa kuzoa taka katika maghuba limetekelezwa
nataka elimisheni wananchi, kaeni nao pamoja ili mshirikiane katika zoezi hili
wakati mwingine wanashindwa kuchangia kwa sababu hamuwashirikishi ipasavyo”,
alisema Dkt. Mahenge.
No comments:
Post a Comment