Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KUFUATIA Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kufunga milango ya Benki
ya Wananchi Mbinga (MCB) isiendelee kufanya kazi wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Serikali (MBINGONET) wilayani humo wamesema
kuwa kufilisika kwa benki hiyo kumesababishwa na viongozi waliopewa dhamana ya
kuiendesha kutokuwa makini na utendaji kazi, usimamizi na utekelezaji wa majukumu
husika.
Aidha MBINGONET wameiomba BOT ifanye uchunguzi wa kina juu ya
suala hilo na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa
Mahakamani, kwani ikumbukwe kuwa MCB ilikuwa ni mkombozi wa wakulima wadogo wadogo
ikiwemo vikundi vya ujasiriamali vilivyopo ndani na nje ya wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Mtandao huo wa mashirika
yasiyokuwa ya serikali wilayani Mbinga, Benedict Luena wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Luena alieleza kuwa imekuwa ni jambo la aibu kwa wanambinga
kupitia vijana wao wasomi ambao waliaminika katika kuendesha benki hiyo lakini hivi
sasa wameshindwa kuiendesha kutokana na kutanguliza mbele maslahi yao binafsi.
“Mtandao huu wa mashirika yasiyokuwa ya serikali wilayani
Mbinga, tumesikitishwa na mfumo uliotumika katika kuiendesha benki ya wananchi
Mbinga hatma iliyopelekea benki hii kufilisika na kufungwa”, alisema Luena.
Alisema kuwa kupitia wanachama wa mtandao huo wameiomba
serikali na vyombo vyake vya uchunguzi isimamie jambo hilo kwa umakini mkubwa ili
hata wateja waliokuwa wa benki hiyo ambao waliweka akiba zao siku ya mwisho waweze
kurejeshewa fedha zao ambazo waliweka katika benki ya MCB.
Katibu huyo wa MBINGONET alidai kuwa inashangaza kuona benki
hiyo jinsi gani ilivyokuwa ikiendeshwa bila kufuata taratibu za kibenki huku
akiongeza kuwa idara ya mikopo ndiyo waliosababisha kushindwa kusonga mbele kwa
benki hiyo kutokana na kile alichodai kuwa na matumizi mabaya ya fedha ambapo
wakati mwingine walikuwa wakitumia fedha pasipo misingi muhimu ya uendeshaji wa
benki.
Alifafanua kuwa matumizi ya uendeshaji wa benki kuwa makubwa
huku wasimamizi husika wakijua kwamba hawaendeshi kwa faida na mwelekeo kwa
baadhi ya watumishi wa benki kujiingizia fedha nyingi katika akaunti zao kwa
njia ya mikopo nalo tatizo hilo limechangia kudorola kwa benki hiyo.
Kwa upande wao nao baadhi ya wateja wa MCB kwa nyakati
tofauti waliongeza wakidai kuwa hata magari yao binafsi wakati mwingine walikuwa
wakitumia fedha za benki hiyo kununulia mafuta na kuweka kwenye magari hayo pasipo
sababu yoyote ile ya msingi kufanya hivyo.
“Pia tulikuwa tukiona wakilazimisha kuchukua fedha za benki
kununulia vifaa mbalimbali wakati mahitaji ya msingi hakuna, kama vile
wanaandikia fedha nyingi kwa ajili ya kununulia vifaa vya stationary wakati
mwingine havihitajiki, sisi tulipokuwa tukihoji kwa nini wanafanya hivi
tulikuwa tunaonekana wabaya,
“Wakati mwingine wanaingia mikataba ya kihuni na makampuni
wanayoyajua wao kwa ajili ya kuchapa kalenda za kila mwaka za benki, utakuta
uchapaji wa kalenda hizi wanaandikia idadi kubwa kwamba wamechapa kalenda kwa
mfano 2,000 wakati kumbe kalenda walizochapa hazijafikia idadi hiyo na hapa
lengo lao ni kutafuta mbinu ya kuiba fedha za benki”, walisema.
Pamoja na mambo mengine, Benki Kuu imeiweka MCB chini ya
mfilisi na kuiteua Bodi ya bima ya amana kama mfilisi, kuanzia Mei 12 mwaka huu
na kwamba uamuzi huo pia umechukuliwa baada ya BOT kujiridhisha kuwa MCB inaupungufu
mkubwa wa mtaji na ukwasi kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki na taasisi za
kifedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.
BOT wakati wanaifunga benki hiyo na kuifutia leseni yake walieleza
kuwa upungufu huo wa mtaji na ukwasi unahatarisha usalama wa sekta ya fedha, hivyo
kuendelea kwake kutoa huduma za kibenki kunahatarisha pia usalama wa amana za
wateja hao.
Vilevile Benki Kuu ya Tanzania imeuhakikishia umma kwamba
itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kutetea
ustahimilivu katika sekta ya fedha ambapo imechukua uamuzi huo wa kuifunga
Benki ya Wananchi Mbinga kwa mujibu wa kifungu cha 56 (1) (g), 56 (2) (a), (b)
na (d), 58 (2) (i), 11 (3) (j), 61 (1) na 41 (a) cha sheria ya mabenki na
taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Hata hivyo BOT imewataka wale wote wenye amana, wadai na
wadaiwa wa iliyokuwa MCB kuwa wavumilivu wakati mfilisi kwa wakati muafaka
atawafahamisha wenye amana, wadai na wadaiwa utaratibu wa malipo wa madai,
ulipaji wa madeni na taratibu nyingine zitakazohitajika kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment