Sehemu ya wajumbe waliohudhuria Mkutano mkuu wa Chama Cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Na Mwandishi wetu,
Dodoma.
MAKAMU wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
amewataka Makatibu Mahsusi hapa nchini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na
kuacha tabia ya kutoa siri za ofisi zao, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Samia Suluhu Hassan alitoa kauli hiyo leo wakati anafungua
mkutano wa tano wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania, kwenye ukumbi wa Jakaya
Kikwete mji Dodoma.
Alisisitiza kuwa uadilifu na uaminifu ndio njia pekee ya
kuaminiwa na viongozi wao, hivyo ni muhimu kwa makatibu hao kufanya kazi kwa
bidii na ubunifu mkubwa katika maeneo yao ya kazi.
Makamu wa Rais pia aliwahimiza makatibu mahsusi kufanya
tathmini ya utendaji wao wa kazi za kila siku na wawe tayari katika kujifunza
mbinu mpya za utendaji zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia.
“Sote tunafahamu kuwa dunia imekuwa ni kijiji kutokana na
utandawazi unaoletwa na mifumo ya teknolojia, hivyo kutokana na mabadiliko haya
hamna budi nanyi kubadilika na kwenda na wakati ili msiangaliwe kwa mtazamo
hasi wa kuwa wapiga chapa tu”, alisema.
Kuhusu uanzishwaji wa Shahada ya Uhazili, Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan amewahakikishia makatibu hao kuwa serikali imekubali
kuanzisha shahada hiyo ambapo masomo yake yataanza mapema mwezi wa tisa mwaka
huu, kwenye Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania katika mikoa ya Dar es Salaam na
Tabora.
Pia amewahimiza kuchangamkia fursa hiyo kwa ajili ya
kujiendeleza kielimu kwa kuzingatia kuwa elimu haina mwisho.
Kwa upande wake, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki alisema kwamba serikali
inafanyia kazi baadhi ya kero zinazowakabili makatibu mahsusi ikiwemo kuboresha
maslahi ya kada ya uhazili nchini.
Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kada hiyo
pamoja na watumishi wengine, wanapata maslahi bora ambayo yatasaidia kwa kiasi
kikubwa katika kuongeza ufanisi wa kazi.
|
No comments:
Post a Comment