Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge
amewataka watumishi wa umma mkoani humo kuwa na subira juu ya madai yao
wanayoidai serikali, kwani watalipwa mara baada ya kukamilika zoezi la uhakiki
wa watumishi wake ambalo linalenga kuwabaini watumishi walioghushi vyeti na
wale wasiokuwa na sifa ambao wanaliingizia taifa hasara kubwa.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa amepiga marufuku tabia ya wakuu
wa idara katika mkoa huo akiwataka kujiepusha kuzalisha madai mapya ya
kuhamisha watumishi kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kuwalipa stahiki
zao.
Dkt. Mahenge alisisitiza kwamba uhamisho kwa mtumishi
yeyote yule ufanyike mara baada ya kulipwa fedha zake za madai ya uhamisho, ili
ziweze kumsaidia kuhama kutoka sehemu alipokuwa anafanyia kazi awali na kwenda
sehemu nyingine hatua ambayo itasaidia kupunguza malalamiko yasiyokuwa ya
lazima.
Agizo hilo la Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge
alilitoa leo wakati alipokuwa akihutubia mamia ya wafanyakazi wa serikali,
taasisi mbalimbali, idara za serikali na sekta binafsi katika sherehe za siku
ya Mei mosi zilizofanyika kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Alisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikisababisha chuki na
uhasama kati ya mtumishi na viongozi wengine huku baadhi yao wakiichukia
serikali yao, jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya wananchi na
moyo wa mtumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
“Kumuhamisha mtumishi pasipokuwa na fedha ya kumlipa
sitaki kusikia tena, jambo hili halikubaliki mahali popote pale nawaonya wakuu
wa idara na taasisi za umma zingatieni kanuni, sheria na taratibu mahali pa
kazi”, alisisitiza Dkt. Mahenge.
Vilevile aliwataka watumishi kuwajibika ipasavyo katika
maeneo yao ya kazi ikiwa ndiyo nguzo muhimu yenye kuleta ufanisi na kwamba
waajiri na waajiriwa nao wanapaswa pia kutambua kuwa kila mmoja anayo haki yake
katika utendaji wa kazi za kila siku.
Alisisitiza kuwa serikali haitafumbia macho kwa mwajiri
yeyote atakayebainika kunyanyasa watumishi wake iwe ni mfanyakazi wa nyumbani,
hotelini, shambani, baa na migodini badala yake kwa yule atakayekiuka taratibu
husika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Pia alisema kuwa kila kiongozi ni lazima atende haki kwa
kufuata sheria na taratibu na kanuni za kazi bila kuingilia majukumu ya mtu
mwingine kwani uwepo wa migogoro sehemu za kazi hasa unyanyasaji
watumishi, hupunguza ari ya kufanya kazi na matokeo yake ni kushuka kwa
ufanisi wa kiutendaji katika taasisi husika.
Aliongeza kuwa wakati huu ambao serikali ya awamu ya
tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kusimamia ufufuaji, uanzishaji
na uimarishaji wa viwanda kila mfanyakazi kwa nafasi yake aliyonayo anatakiwa
kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuweza kukuza uchumi wa nchi.
Dkt. Mahenge alieleza kuwa katika awamu hii Rais Dkt.
Magufuli kupitia kauli mbiu yake ya Hapa kazi tu, amekuwa akisimamia kwa dhati
uchumi wa nchi ya Tanzania uweze kukua kwa kuendelea kujenga viwanda vya aina
mbalimbali vya kuzalisha mali ikiwemo viwanda vidogo, vya kati na hata vikubwa
ambavyo vitasaidia kuongeza kipato na ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wao wafanyakazi ndani ya mkoa huo kupitia
risala yao iliyosomwa na Theresia Tonya wameahidi kuiunga mkono serikali ya
awamu ya tano kwa kuongeza juhudi maeneo yao ya kazi ili kuleta tija kwa lengo
la kuharakisha ukuaji wa maendeleo hapa nchini.
Hata hivyo Tonya alisema wanaunga mkono hatua mbalimbali
anazochukua Rais huyo hasa kwa watumishi wasiokuwa na sifa ambao wameajiriwa
serikalini wamekuwa wakiibia serikali kwa njia ya kulipwa mishahara huku
wakijua kwamba wanakiuka taratibu na sheria za utumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment