Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa hali ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa
wa Malaria kwa akina mama Wajawazito, Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma katika kipindi cha mwaka 2016/2017 imefikia kuwa ni asilimia 1.9 na kwa
upande wa Watoto chini ya miaka mitano ni asilimia 9.6 ambapo halmashauri hiyo
inaendelea na mikakati mbalimbali ya mapambano dhidi ya kuutokomeza ugonjwa
huo.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye alisema hayo
juzi alipokuwa akisoma risala ya utii wa wananchi wa halmashauri ya mji wa
Mbinga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ambayo
ilisomwa mbele ya kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Amour Hamad Amour
katika viwanja vya Masumuni mjini hapa.
Nshenye alisema kuwa mapambano
hayo dhidi ya ugonjwa wa Malaria wamejipanga kikamilifu kwa
kuhakikisha wanatekeleza,
elimu ya Kinga dhidi ya ugonjwa huo inaendelea kutolewa kwa wananchi ambapo mpaka sasa jumla ya kata 19 na vijiji 49 vimefikishiwa elimu husika ikiwemo kufanya usafi wa
mazingira na matumizi sahihi ya vyandarua.
Alisema kuwa jumla ya vyandarua
1,681 vimegawiwa kwa
akina mama wajawazito na watoto waliochini
ya umri wa miaka mitano
ambapo huduma hiyo imekuwa ikitolewa kwa kundi hilo pale wanapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza.
“Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje hapa
wilayani tumeendelea na kampeni maalum ya kupambana na malaria kama vile kutoa elimu, kuhamasisha kusafisha mazingira, kupima na kutoa tiba ya ugonjwa huu,
“Wananchi wamekuwa wakiendelea
kuhamasika katika kupambana na Malaria kwa kusafisha mazingira ya makazi, matumizi
sahihi ya vyandarua na Kuzingatia huduma ya matibabu dhidi ya ugonjwa huu”, alisema Nshenye.
Pia alibainisha kuwa makundi
maalum nayo yamekuwa yakishirikishwa katika kampeni na programu za kupambana na ugonjwa huo kupitia mikutano ya hadhara, matamasha au mikusanyiko
maalum na sherehe za maazimisho mbalimbali.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Amour Hamad Amour alipongeza jitihada hizo zinazofanywa na kutaka ziendelezwe
ili kuweza kufikia malengo ya kuutokomeza ugonjwa huo ambao ni hatari katika
jamii.
Vilevile Amour alisema kuwa taifa lenye nguvu ni lile ambalo
watu wake wana afya bora hivyo wananchi wanapaswa kuzingatia kanuni bora za
afya na tiba ili kuweza kufikia nyanja bora ya kimaendeleo kwa faida ya kizazi
cha sasa na kile kijacho.
No comments:
Post a Comment