DAKTARI Mshauri kutoka Chama cha Afya ya Jamii Tanzania (TPHA) Dkt. Ali Mzige amewataka Watanzania kuepuka uzito mkubwa na kitambi ili kufanya miili yao kukaa mbali na magonjwa yanayosababishwa na vitu hivyo.
Aidha Dkt. Mzige amezungumza hayo leo katika ukumbi wa maelezo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakichukulia kawaida na wengine wanapenda kuwa na kitambi na uzito mkubwa, lakini ni vitu vyenye madhara makubwa na husababisha magonjwa ambayo ni magumu kutibika.
“Unene uliokithiri huleta shida kwenye moyo, shinikizo kubwa la damu, kisukari, saratani za aina mbalimbali, kushindwa kupumua vizuri na magonjwa mengine mengi hivyo watu wanatakiwa kuepuka ili kujinusuru na magonjwa hayo”, alisema Dkt. Mzige.
Aliongeza kuwa tafiti zinaonesha kuwa asilimia kubwa wanawake wanavitambi na uzito uliokithiri kuliko wanaume hali inayotokana na wanawake wengi kupendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi.
Hivyo aliwataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kula vyakula vya asili, kufanya mazoezi na kupima afya zao mara kwa mara ili kujua mapema kama ana tatizo lolote la kiafya na kujiepusha na maradhi yanayoweza kuepukika.
Pia alifafanua kwamba uzito wa mtu unatakiwa kulingana na umri na urefu wake kwani mtoto wa mika 5 anapaswa kuwa na kilo 18, kijana mwenye miaka 14 mvulana kilo 48 na msichana kilo 49 huku mtu mzima mwanaume mwenye urefu wa futi 5 na inchi 8 anapaswa kuwa na kilo 68.
Tiba nzuri na iliyosahihi ya kuepuka maradhi mengi ni kutokaa masaa manne bila kufanya kazi, kuzuia kitambi kisijitokeze kwa kula kiasi cha chakula kinacholingana na mahitaji yako, kupunguza ulaji wa sukari na mafuta na kuepuka unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara.
No comments:
Post a Comment