Na Dustan Ndunguru,
Geita.
WACHIMBAJI wadogo wa madini katika migodi ya Kakola na
Nyakagwe wilaya ya Kahama na Geita mkoani Geita, wamesema kuwa uamuzi aliochukua
Rais Dkt. John Magufuli wa kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza Makontena yenye
mchanga wenye madini ulikuwa ni wa busara kutokana na ukweli kwamba mchanga huo
uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi, ulikuwa wenye madini jambo ambalo
lilikuwa likisababisha nchi kukosa mapato yake.
Dkt. John Magufuli. |
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi
wachimbaji wadogo, Robert Nyamaigolo na Golod Makinga walisema kuwa kila Mtanzania
ambaye ana uzalendo wa kweli anapaswa kupongeza jitihada hizo zilizofanywa na
Dkt. Magufuli baada ya kumaliza kazi hiyo na kuchukua hatua.
Nyamaigolo alisema uzoefu unaonesha kuwa miaka mingi tume za
kuchunguza masuala mbalimbali zilizokuwa zikiundwa zilikuwa hazitoi majibu
yenye kuzaa matunda na baadaye wananchi walikuwa wakikosa imani na serikali
yao.
“Rais Magufuli ameunda tume ya kuchunguza tatizo hili, mara
ilipobainika kulikuwa na uzembe kwa watendaji husika ambao wameufanya mara moja
amechukua hatua ya kuwawajibisha, ni jambo ambalo anapaswa kupongezwa hasa kwa
Watanzania ambao ni wazalendo na wenye uchungu na rasilimali za nchi yao”,
alisema Nyamaigolo.
Nyamaigolo alifafanua kuwa ni miaka mingi imepita Makontena
yenye mchanga wa madini yalikuwa yakisafirishwa kwenda nje ya nchi, ambapo wao
kama wachimbaji wadogo hawakuwa na sauti ya kulizungumzia hilo kutokana na
ukweli kwamba wawekezaji kwenye migodi hiyo walikuwa wamepewa kibali cha
kusafirisha mchanga huo wenye madini.
“Sisi kama wachimbaji wadogo tuna ushahidi wa kutosha
kuhusiana na mchanga huu uliokuwa ukisafirishwa kwa muda mrefu kabla hata Rais Dkt.
Magufuli hajasitisha kusafirishwa huku, kilichotupatia uhakika ni kwamba madini
yalikuwa yanaondoka huku tukiyaona kwa macho yetu na vilevile ni kile kitendo
cha Kontena moja lenye mchanga kudondoka na mchanga wenye madini katika eneo la
Segese huko Kahama”, alisema Nyamaigolo.
Alibainisha kuwa mara baada ya Kontena hilo kudondoka,
wachimbaji wadogo walikuwa wakiuziwa mchanga ambapo walikuwa wakiendelea na
kazi ya uchakataji ambapo kilichotokea katika mchanga huo, waliweza kupata
dhahabu ya kutosha na ndipo walipokuwa na uhakika wa kile ambacho
kinasafirishwa ni madini ya dhahabu na sio vinginevyo.
Mchimbaji huyo alieleza kuwa hata kabla ya Kontena hilo
kudondoka madereva waliokuwa wakiendesha Makontena yenye mchanga wa madini walikuwa
wakiwauzia mchanga huo wachimbaji wadogo kulingana na kiasi cha fedha walichonacho
na kuweza kujipatia dhahabu.
Nyamaigolo alisema kuwa kutokana na hilo ni vyema serikali
ikawashirikisha wachimbaji wadogo pale ambapo panahitajika kufanya uchunguzi kuhusiana
na jambo lolote lile linalohusu madini, hususan katika sakata la sasa la
usafirishaji wa mchanga wenye madini na kwamba Watanzania wanapaswa pia kufahamu
wazi kuwa ni kweli nchi ilikuwa ikiibiwa madini mengi.
Naye Golod Makinga aliwaasa Watanzania kuunga mkono jitihada hizo
zinazofanywa na Rais Dkt. Magufuli katika kupambana na wale wote ambao kwa
miaka mingi walikuwa wakinufaika na rasilimali zilizopo hapa nchini kwa njia ya
isiyo halali na kuwaacha wengi wakiwa maskini na kwamba aliiomba serikali
kutoruhusu tena mchanga wenye madini kusafirishwa kwenda nje ya nchi badala
yake kila jambo lifanyike ndani ya nchi kwa lengo la kuongeza mapato na ajira.
Makinga aliongeza kuwa serikali inaowajibu wa kuhakikisha kwamba
inaendelea kuwalinda wachimbaji wadogo kutokana na ukweli kwamba hiyo ndiyo ajira
yao ambayo imekuwa ikiwafanya waweze kuendesha maisha yao ya kila siku na isisite
kuwaunga mkono kwa kuwapatia vifaa vya kisasa ambavyo vitawasaidia katika
shughuli zao za uchimbaji wa kila siku.
No comments:
Post a Comment