Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Watumishi wa Manispaa ya Songea (Hawapo pichani) katika ziara ya siku moja ya kukagua usafi wa mazingira katika mji wa Songea mkoani humo. |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
SERIKALI mkoani Ruvuma, imetoa agizo kwa kumtaka Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani humo, Tina Sekambo
kuwalipa fidia shilingi milioni 22 wakazi wa kata ya Subira katika Manispaa
hiyo, ambao eneo lao lenye ekari 25 limetwaliwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa
dampo la kisasa la kuhifadhia taka.
Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith
Mahenge wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Manispaa hiyo katika ziara
yake ya siku moja ya kukagua maghuba ya kuhifadhia taka yaliyopo mjini hapa.
Kadhalika Dkt. Mahenge alisema
kuwa wakati Manispaa inatekeleza taratibu za ujenzi wa dampo hilo kuna kila
sababu pia ya kutafuta eneo lingine maalum kwa muda nje ya mji huo kwa ajili ya
kumwaga taka hizo zinazozalishwa hivi sasa.
Vilevile Mstahiki Meya wa Manispaa
hiyo, Abdul Mshaweji akizungumzia hilo amemuhakikishia Mkuu wa mkoa huyo kutekeleza
agizo hilo mapema ambapo alisema Manispaa ina maeneo mawili nje ya mji huo, ambayo
yataweza kutumika kwa muda kutupa taka wakati maandalizi mengine ya ujenzi wa
dampo hilo la kisasa unafanyika.
Awali akisoma taarifa ya hali ya
uzalishaji taka katika mji wa Songea Tina Sekambo ambaye ni Mkurugenzi mtendaji
wa Manispaa hiyo alisema kuwa Manispaa imekuwa ikizalisha taka kiasi cha tani
71.5 kwa siku, huku uwezo wa kuzoa taka hizo kwa siku ukiwa ni kati ya tani 35
hadi 40 hali ambayo inasababisha tani 31.5 kubaki bila kuzolewa.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa tangu
mwezi Januari mwaka huu Manispaa imekosa sehemu maalum ya kutupa taka kutokana
na wananchi wa Mwengemshindo ambako taka zilikuwa zinatupwa hapo awali, kuzuia
magari yasimwage tena taka huko hivyo kufanya zoezi hilo lisimame kwa muda
utekelezaji wake.
Kwa upande wake Ofisa usafi na mazingira
wa Manispaa ya Songea, Philipo Beno alisema Manispaa hivi sasa wana jumla ya maghuba
33 ya kuhifadhia taka katika mji huo.
“Idara inatarajia hivi karibuni
kupokea kijiko yaani mtambo wa kuzolea taka ambao utarahisisha ukusanyaji wa
taka hizi na kupunguza muda wa kuzoa kwa urahisi zaidi”, alisema Beno.
No comments:
Post a Comment