Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HATIMAYE Diwani wa kata ya Kitanda, Zeno Mbunda Halmashauri
ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma amejikuta akiendelea kuwa katika wakati mgumu
baada ya kusimama mbele ya kikao maalumu na kuwaomba radhi baadhi ya Wananchi
na Wajumbe wa Baraza la maendeleo la kata hiyo, huku akikiri kwamba tuhuma
anazotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa mali na fedha za wananchi hao kuwa ni za
kweli.
Zeno Mbunda, Diwani kata ya Kitanda. |
Pamoja na diwani huyo kukubali makosa hayo mbele ya kikao
hicho kilichofanyika Juni 17 mwaka huu kwenye Ofisi za makao makuu ya kata ya
Kitanda, aidha alieleza kuwa ifikapo Julai Mosi mwaka huu atakuwa amelipa mali
na fedha zote ambazo anadaiwa kutofikisha katani humo.
Radhi hiyo ambayo alikuwa akiiomba mbele ya ushuhuda wa viongozi
wa CCM wilaya ya Mbinga, akiwemo na Mwenyekiti wa Chama hicho Christantus
Mbunda ambaye alikuwa akiongoza kikao hicho.
Licha ya kuwaomba radhi bado Wajumbe wa baraza hilo la
maendeleo la kata walionekana kutoridhishwa na hali hiyo huku wengine wakisema
kuwa hawawezi kuchukua hatua ya kumsamehe, kwani ni mapema mno mpaka pale
atakaporejesha mali na fedha za wakulima wa kahawa anazotuhumiwa kuzitafuna kwa manufaa yake binafsi.
“Hatuwezi kuchukua hatua ya kumsamehe mpaka pia tupate majibu
ya hatua zilizochukuliwa kutoka Ofisi ya Mkuu wa wilaya, ambako malalamiko haya
tuliyapeleka kwa njia ya maandishi na bado hatujajibiwa mpaka sasa”, alisema
Mwenyekiti wa kata ya Kitanda Philibert Mkolwe.
Mkolwe aliongeza kuwa hawaoni sababu ya kuendelea kuwa na
kiongozi ambaye ni mwizi wa mali za wananchi ni vyema achie madaraka kwani
mpaka sasa amesababisha kupungua kwa moyo wa kufanya shughuli za maendeleo
ndani ya kata.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya
Mbinga, Christantus Mbunda akizungumza katika kikao hicho maalumu ambacho
kililenga kutafuta suluhisho la mgogoro huo, licha ya kuwasihi Wajumbe wa
mkutano huo wamsamehe diwani wao hali ilizidi kuwa mbaya ambapo waliendelea
kujenga msimamo wao wakieleza kuwa hawawezi kumsamehe mtu ambaye ananyoshewa
kidole kufanya ubadhirifu wa mali za umma.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa anakubaliana na Wajumbe hao
kwamba anapaswa kulipa kwanza mali na fedha za wananchi ndipo wamsamehe kwa
kupita tena katika kila vijiji vilivyopo kwenye kata hiyo kwa kufanya mikutano na
wananchi hao kuwaomba radhi kwa makosa aliyowafanyia.
Kufuatia uwepo wa hali hiyo, Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya
aliongeza kuwa kuanzia sasa diwani huyo hatakiwi kuonekana tena anashiriki
kwenye shughuli za manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa miradi ya maendeleo ya
wananchi, badala yake anapaswa kumwachia Afisa mtendaji wa kata hiyo ambaye
ndiye mhusika mkuu wa kusimamia shughuli hizo na yeye anabakia kuwa ni
mfuatiliaji wa shughuli hizo kuona kama zinatekelezwa ipasavyo au la.
Pamoja na mambo mengine, hapo awali kufanyika kwa kikao hicho
kunafuatia hatua ya Wajumbe hao kumkataa diwani Mbunda, baada ya kutoa
malalamiko yao kwa kuandika barua kwenda Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga,
wakimtuhumu kufanya ubadhirifu huo wa mali za wananchi wake.
Barua hiyo ya malalamiko iliyoandikwa Mei 25 mwaka huu ambayo
nakala yake tunayo ikiwa na majina na sahihi za mahudhurio ya Wajumbe hao,
wameiomba serikali ichukue hatua dhidi ya kiongozi huyo kwa lengo la kuweza
kunusuru maendeleo ya wananchi wa kata hiyo.
Sehemu ya barua hiyo inasema kuwa kutokana na kikao cha
baraza hilo la kata ya Kitanda kilichofanyika kwa pamoja, walikubaliana
kutomuamini tena diwani wao na kumkataa kwa sababu ya kupokea mipira (Roll)
kumi ya maji kutoka kwenye mfuko wa Jimbo la Mbinga mjini na kutowasilisha kwa
wananchi wa kitongoji cha Matengo kijiji cha Masimeli kwa ajili ya ujenzi wa
mradi wa maji.
Pia wanamtuhumu kufanya upotevu wa vifaa vya ujenzi ambavyo
ni saruji, nondo na bati za kuezekea baadhi ya majengo katika shule ya
Sekondari Ngwilizi iliyopo katika kata hiyo, vifaa ambavyo vilitolewa na mfuko
huo wa jimbo kupitia usimamizi wake na kusababisha vifaa hivyo kupelekwa
shuleni hapo vikiwa pungufu huku wakidai pia alipokea msaada wa fedha taslimu
shilingi milioni 2 toka kwa Shirika la Masista wa Chipole lililopo wilayani
hapa na kutozifikisha kwa Kamati ya ujenzi ya shule hiyo ya Sekondari ili
ziweze kusaidia katika kazi ya ujenzi.
Vilevile wanadai kuwa diwani huyo wa CCM ameshiriki kukusanya
kahawa ya wakulima kupitia kikundi cha Mjimwema kilichopo kwenye kijiji cha
Masimeli, msimu wa mavuno ya zao hilo mwaka 2016/2017 na kutowapa malipo yao wakulima
hao baada ya kuiuza kahawa yao ambayo ni zaidi ya tani kumi.
No comments:
Post a Comment