Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida, wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro alipowatembelea katika kuadhimisha wiki ya utumishi umma. |
Na Mwandishi wetu,
Singida.
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt.
Laurean Ndumbaro amewataka viongozi na watumishi wote hapa nchini, kuzingatia
nidhamu na maadili ya utumishi wa umma ikiwa ndiyo msingi bora wa utendaji kazi
ili utumishi wao uweze kuwa mzuri.
Dkt. Ndumbaro alisema hayo leo alipokutana na watumishi wa mkoa
wa Singida na kusikiliza matatizo, kero, changamoto pamoja na kupata maoni ya
namna ya kuboresha utumishi wa umma kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya
utumishi wa umma nchini.
Alisema kuwa kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa bidii na
nidhamu ya hali ya juu huku akisisitiza viongozi hasa wa watumishi wa umma,
kuwasikiliza watumishi wao pale wanapotoa maoni yao bila kuyapuuza au
kuwakatisha tamaa kwa vitisho.
“Ukiwa kiongozi unapaswa uweze kuishi na kila aina ya mtu,
kuna watumishi wengine hawawezi kufichaficha mambo ukikosea wanakusema bila
kupepesa maneno, wengine ni waoga hawawezi kukueleza wazi ila wanatumia mbinu
mbalimbali, ukiwa kiongozi uwe tayari kupokea ushauri ili uweze kuboresha
utendaji wako”, alisisitiza Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro aliwaasa viongozi hao kuwapongeza watumishi
wanaofanya kazi kwa bidii na wenye nidhamu ili iwe motisha kwa wale wavivu,
huku akiwataka kuwachukulia hatua wale wazembe ambao hawataki kufuata kanuni na
maadili ya utumishi wa umma.
“Unakuta mtumishi anajituma anafanya kazi kwa bidii ana
nidhamu na ni mbunifu lakini wewe kiongozi wake unamuangalia tu bila hata ya kumpongeza
hiyo inakatisha tama, inatakiwa umpongeze sio lazima umpe fedha hata barua tu
ya kutambua utendaji wake itampa hamasa yeye na wenzake lakini pia kuna
mwingine anakuwa hatekelezi wajibu wake unamtazama tu, hapo utawakatisha tamaa
hata wale wachapakazi wengine”, alisema.
Aidha aliwapongeza watumishi wenye vyeti halali huku akieleza
kuwa zoezi la uhakiki wa watumishi bado ni endelevu ili kuhakikisha kwamba watumishi
wanaobaki serikalini ni wale wanaostahili tu huku akiwashauri watumishi
kuhakikisha wanasafisha taarifa zao muhimu ziwe halali na sahihi wakati wote.
Naye Katibu tawala mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi alimshukuru
Katibu Mkuu Utumishi wa umma, Dkt. Ndumbaro kwa kuwatembelea watumishi wa mkoa
wa Singida na kusikiliza changamoto pamoja na maoni yao huku akiahidi kwa niaba
ya watumishi kwamba wataendelea kuchapa kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya
juu.
Dkt. Lutambi alisema watumishi mkoani Singida wanaadhimisha
wiki ya Utumishi wa umma, kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuongeza muda wa
kufanya kazi kutoka saa tisa na nusu mchana mpaka saa kumi na nusu jioni ili
kutoa muda zaidi wa kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya
ya Iramba Linno Mwageni, naye alimshukuru Katibu Mkuu huyo Utumishi wa umma kwa
kutembelea mkoa wa Singida na kutoa maoni yake ili kuboresha utendaji hasa wa
serikali za mitaa na kwamba alieleza kuwa serikali inabidi iwaajiri watendaji
wa vijiji na kata wa kutosha ili kuweza kuleta ufanisi katika utendaji kazi kwenye
maeneo hayo.
Mwageni alisema kuwa wanaotekeleza shughuli na miradi ya
serikali kwa ngazi ya mwananchi hasa maeneo ya vijijini na kata ambao hivi sasa
ni wachache ni hao watendaji hivyo serikali haina budi kuwaajiri wengine ili
waweze kutosheleza katika maeneo hayo hasa katika ufuatiliaji wa miradi ya
maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment