Na Mwandishi wetu,
Nyasa.
KUFUATIA uwepo wa samaki wengi wa mapambo katika ziwa
Nyasa mkoani Ruvuma, serikali imejiwekea mkakati wa kuifanya wilaya ya Nyasa
mkoani humo kuwa ndiyo kivutio cha utalii na uwekezaji, kutokana na wilaya hiyo
kuwa katika mazingira mazuri yanayovutia watalii wa kutoka ndani na nje ya
maeneo mbalimbali wilayani hapa.
Uwepo wa sifa hizo katika ziwa hilo, linatajwa pia
kuwa na samaki wa mapambo zaidi ya 320 ambao wengine hutumika kwa kitoweo cha
binadamu.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith
Mahenge alipokuwa akizungumza na Wananchi wa kata ya Mbamba bay na Wadau wa
mazingira wilayani Nyasa, wakati akiongoza shughuli za usafi wa
mazingira katika maeneo mbalimbali.
Dkt. Mahenge alisema kuwa kutokana na baadhi ya
wananchi wamekuwa wakionekana kutofahamu umuhimu wa ziwa hilo, jambo hilo limekuwa
likichangia na kusababisha kukwamisha mkakati wa maendeleo ya utangazaji wa
vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.
Hivyo basi, aliwataka viongozi wa wilaya kwa ujumla kuhakikisha
kwamba wanaweka mkakati kabambe na endelevu katika suala zima la usafi wa mazingira
kwenye maeneo yote na kutolifanya suala hilo kuwa la kisiasa.
Alisema kuwa hataweza kufanikiwa mkakati wa kuifanya
wilaya ya Nyasa inakuwa na kituo cha vivutio vya utalii na uwekezaji, endapo hakutakuwa
na mazingira mazuri yanayoshawishi watu kwenda na kupenda kuwekeza katika
shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Bila kuwa na mazingira rafiki ni vigumu kwa mkoa kufanikisha
jambo hili ni vyema sasa wananchi wa Nyasa watambue kuwa wilaya
yao ni muhimu kuboresha masuala ya uwekezaji, hivyo wananchi na
viongozi wanalojukumu kubwa la kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli
hii ili kuweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi”, alisema.
Aliongeza kuwa binadamu na shughuli zao, kila siku wamekuwa
wakiongezeka lakini mazingira yaliyopo duniani hayawezi kuongezeka hivyo kuna
umuhimu mkubwa kwa binadamu kutunza rasilimali zilizopo ili zisiweze kuharibiwa
kwa faida ya sasa na baadaye.
Kwa mujibu wa Dkt. Mahenge alieleza kuwa madhara ya
uharibifu wa mazingira hayo ni pamoja na kukosekana kwa mvua ambazo binadamu
hutegemea kwa kuendesha maisha yake ikiwemo shughuli za kilimo ili aweze
kujipatia mazao ya chakula na biashara.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa amewataka
wananchi wilayani humo kuongeza pia kasi ya upandaji miti kwenye maeneo yao ambayo
ni rafiki ya mazingira katika utunzaji wa maji ardhini.
No comments:
Post a Comment