Na Mwandishi wetu,
Songea.
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani
Ruvuma, limemfukuza kazi Afisa maendeleo ya jamii wa wilaya hiyo, Wenisalia
Swai kutokana na kubadili matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa
jengo la Ofisi ya halmashauri hiyo bila kufuata taratibu husika.
Aidha Swai anadaiwa kutenda kosa la kubadili fedha shilingi
milioni 130 zilizotolewa na ubalozi wa Japan hapa nchini, kwa ajili ya
kuboresha kituo cha afya Mhukuru kilichopo wilayani humo kwa kumlipa
mkandarasi aliyejenga jengo la halmashauri katika kijiji cha Lundusi kata ya
Maposeni, wakati fedha kwa ajili ya ujenzi huo zilikwishatolewa na serikali.
Pia mtumishi huyo imeelezwa kuwa alibadili matumizi ya fedha
nyingine zaidi ya shilingi milioni 156 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa
Skimu ya umwagiliaji katika kijiji cha Nakahuga na kuzielekeza kwenye utengenezaji
wa madawati na ujenzi wa jengo la maabara, jambo ambalo limesababisha wakulima
wa kijiji hicho kushindwa kuendesha na kunufaika na mradi huo wa umwagiliaji.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Songea, Simon
Bulenganija alisema kuwa, Swai alipokuwa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo
kabla ya Rais Dkt. John Magufuli hajateua wakurugenzi wa halmashauri za wilaya,
miji, manispaa na majiji mwaka jana kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi
wengine akiwemo Mweka hazina wa halmashauri hiyo, Mwajuma Sekelela na Mkuu wa kitengo
cha manunuzi Amina Njogela walibadili matumizi ya fedha hizo bila kupata idhini
ya Kamati husika ya fedha, mipango na uchumi.
Akizungumza na mwandishi wetu jana Ofisini kwake
mara baada ya kumalizika kwa baraza maalumu la kinidhamu, Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo, Bulenganija alieleza kuwa awali watumishi hao wote
watatu tayari walikwisha simamishwa kazi miezi minne iliyopita kwa lengo la
kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma hizo, hasa baada ya kubainika kwamba
walichukua maamuzi ya kutumia fedha hizo kama mali yao binafsi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa mbali na
kufukuzwa kazi Afisa maendeleo huyo, baraza hilo kwa pamoja limekubaliana
kumshusha cheo Mweka hazina wa halmashauri, Mwajuma Sekelela baada ya
kupatikana na kosa la kushiriki na kupitisha ubadilishaji
wa matumizi ya fedha hizo hatua ambayo ilisababisha madiwani hao
kuwa na mashaka naye.
Kadhalika baraza hilo limemrudisha kazini Mkuu wa kitengo cha
manunuzi, Amina Njogela ambaye naye alisimamishwa kazi na wenzake kwa kosa la
kushiriki katika maamuzi ya kubadilisha matumizi ya fedha hizo na kuchelewesha
mchakato wa ujenzi wa Skimu hiyo ya umwagiliaji kijiji cha Nakahuga.
Hata hivyo Bulenganija alitoa wito kwa watumishi wengine wa
halmashauri ya wilaya ya Songea kuwa waadilifu na waaminifu katika majukumu yao
ya kazi za kiutumishi kila siku kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za
utumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment