Na Mwandishi wetu,
Songea.
WATU watatu wamefariki dunia katika
matukio mawili tofauti likiwemo la wawili kufa papo hapo, baada ya gari
lililokuwa na tela lake likiwa limesheheni makaa ya mawe kuacha njia na
kupinduka kisha kutumbukia katika mto Nakatete uliopo Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma.
Akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake,
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Gemin Mushy aliwataja waliofariki dunia kuwa ni
Shaban Msangi (39) ambaye alikuwa ni dereva wa gari hilo lililobeba makaa ya
mawe, Haji Yusuph (18) alikuwa ni tingo wa gari hilo wote ni wakazi wa Manispaa
ya Mtwara Mikindani na Cosmas Thadei (80) mkazi wa eneo la Sanangula Manispaa
ya Songea.
Alifafanua kuwa katika tukio la kwanza inadaiwa kuwa Juni
20 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji cha Utwango kata ya Namabengo
wilayani Namtumbo, gari lenye namba za usajili T 767 DKS lililokuwa na tela
lake lenye namba za usajili T 324 DKS aina ya HOWO mali ya Kampuni ya Dangote
lilikuwa limebeba tani 25 za makaa ya mawe likitokea Songea kwenda Mtwara.
Gari hilo lilikuwa linaendeshwa na Msangi ambapo
lilikuwa kwenye mwendo kasi liliacha njia na kupinduka, kisha kutumbukia kwenye
mto huo ambao upo Kilometa 30 kutoka katika Manispaa ya Songea na kusababisha
vifo hivyo vya watu wawili.
Alilitaja tukio jingine kuwa Juni 20 mwaka huu majira ya
saa 3 usiku katika eneo la Sanangula kwenye barabara ya kutoka Songea kwenda
Njombe, Pikipiki yenye namba za usajili MC 871 ABA aina ya Sanlg iliyokuwa ikiendeshwa
na dereva ambaye jina lake halikuweza kufahamika ilimgonga mtembea kwa miguu,
Cosmas Thadei mkazi wa eneo hilo na kusababisha kifo papo hapo na dereva wa
Pikipiki hiyo baada ya kubaini amesabisha kifo alikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Miili ya marehemu hao watatu hivi sasa imehifadhiwa
katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya mkoa wa Ruvuma Songea, ikisubiri ndugu
wajitokeze kwenda kuichukua kwa ajili ya mazishi na kwamba Jeshi la Polisi mkoani
humo linaendelea kumtafuta mwendesha bodaboda huyo ambaye amekimbia na
kuitelekeza Pikipiki yake.
Kwa ujumla imefafanuliwa kuwa chanzo cha ajali zote
mbili ni mwendo kasi ambao ulisababisha madereva hao kushindwa kudhiti vyombo
vyao vya moto wakati walipokuwa wakiendesha.
No comments:
Post a Comment