Na Muhidin Amri,
Songea.
WAKAZI wanaoishi katika mtaa wa Ruhuwiko Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, wameondokana na kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi
na salama baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa tanki la maji
katika mtaa huo ambalo sasa husambaza maji hayo katika maeneo mbalimbali
wanayoishi.
Abdul Mshaweji. |
Aidha katika hatua nyingine wametakiwa kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na serikali hii ya awamu ya tano katika kumaliza kero
wanazokabilianazo wananchi wake.
Sambamba na hilo wamekumbushwa pia wajibu wao wa kuisaidia
serikali juu ya mkakati wa kuinua uchumi wao kwa kubuni miradi ya
maendeleo ambayo itawaingizia kipato kuanzia ngazi ya familia.
Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji alitoa
kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa mtaa huo, katika
mkutano wa hadhara ulioitishwa na wananchi hao wakilenga kuishukuru serikali
kwa kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa maji katika mtaa huo wa Ruhuwiko.
Mshaweji alisema kuwa ameiagiza kamati inayosimamia mradi huo
kuhakikisha kwamba inajiepusha na vitendo vya upendeleo katika kuendesha mradi
huo badala yake wahakikishe kwamba, kila mwananchi anachangia na kulipia bili
za matumizi ya maji kila mwishoni mwa mwezi ili uweze kuwa endelevu na
kuwezesha kupatikana fedha kwa ajili ya kuufanyia matengenezo hasa pale linapotokea
tatizo la kuharibika mabomba ya kutolea maji.
“Natambua matatizo ya baadhi ya wananchi kutokuwa na mwamko
wa uchangiaji fedha katika huduma mbalimbali za kijamii, lakini nawasihi wakazi
wa eneo hili muwe mfano wa kuigwa kwa kuchangia huduma hii ili iweze kuwa
endelevu”, alisisitiza Mshaweji.
Pamoja na mambo mengine kwa nyakati tofauti wananchi wa mtaa
wa Ruhuwiko walipozungumza na mwandishi wetu, walisema kuwa wanatambua mchango
huo uliotolewa na serikali kwamba imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa mradi
huo hivyo wanaishukuru na kwamba wataendelea kutekeleza kwa vitendo yale yote
ambayo wanapaswa kuyatekeleza katika kuuendeleza mradi huo wa maji.
No comments:
Post a Comment