Washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea na mafunzo katika ukumbi wa Dear Mama uliopo mjini Dodoma. |
Kassian Nyandindi na Magesa Magesa,
Dodoma.
IMEELEZWA kuwa mafunzo ya utangazaji ambayo
yanaendeshwa kwa Waandishi wa habari mkoani Dodoma, yataweza kuwasaidia
wanahabari hao katika kufanya kazi zao kwa weledi na misingi bora ambayo
itawafanya waendane na zama hizi za Sayansi na tekinolojia.
Hayo yalisemwa jana na Mjumbe wa Kamati ya maadili
kutoka Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Salma Abdul
wakati alipokuwa akifungua mafunzo hayo ya siku nne, ambayo yamefadhiliwa na umoja huo yanayofanyika kwenye
ukumbi wa hoteli ya Dear Mama iliyopo mjini hapa.
“Sisi ni watu ambao tutakuwa bora zaidi kutokana na
utangazaji wetu kuwa mzuri ukizingatia kwamba hivi sasa mtangazaji ndio kila
kitu, hivyo tunapaswa wakati wote kuzingatia maadili ya kazi zetu”. alisema
Salma.
Vilevile kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo,
Dotto Bulendu kutoka Chuo kikuu cha SAUT mkoani Mwanza alisema kuwa kutokana na
watu wa redio kuwa na ushindani mkubwa na watu wa televisheni, waandishi wa
habari wanapaswa kuendana na wakati kwa kuwa wabunifu zaidi katika kuandika
habari zao.
Bulendu alisema kuwa ubunifu huo endapo watazingatia
katika ufanyaji wa kazi zao za kila siku utasaidia kuwafanya wasikilizaji
kupenda zaidi kusikiliza habari zao kwa kuwa zitakuwa zimezingatia maadili na
misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.
“Unapoandika habari yako ni lazima uzingatie
wasikilizaji wako wanahitaji nini na ili iweze kuwa na matokeo mazuri lazima
uzingatie haya tunayojifunza sasa, bila kusahau ubunifu mzuri wa maneno ambayo
yatafikisha ujumbe mzuri kwa jamii”, alisisitiza Bulendu.
Hata hivyo washiriki waliopo katika mafunzo hayo ni wa
kutoka katika Klabu za waandishi wa habari mikoa ya Ruvuma, Morogoro, Dar es
Salaam, Zanzibar, Dodoma, Simiyu, Singida, Arusha, Geita, Kagera, Mtwara, Mara,
Tabora na Lindi.
No comments:
Post a Comment