Thursday, June 8, 2017

KUKAMILIKA MRADI WA MAJI LIGANGA KUTAWANUFAISHA WANANCHI

Na Julius Konala,    
Songea.

ENDAPO mradi wa maji ya mtiririko unaojengwa katika kijiji cha Liganga halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma utakamilika ujenzi wake, wananchi waishio kwenye kijiji hicho wataweza kunufaika na kuondokana na adha ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Mradi huo ambao umefadhiliwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Misheni Peramiho, Dkt. Ansgar Stuffe (OSB) mkoani hapa, utagharimu shilingi milioni 270 mpaka kukamilika ujenzi wake.

Uzinduzi wa mradi huo umefanywa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi huyo kwa kufunga Koki 60 za maji ya mtiririko, katika maeneo mbalimbali ya kijiji hicho wilayani humo.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mradi huo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa ameamua kuwafadhili mradi huo wananchi wa kijiji cha Liganga kutokana na kuguswa na changamoto ya tatizo la ukosefu wa maji ambalo linawasumbua wananchi hao kwa muda mrefu.

“Nimefurahi kuona mradi huu nilioufadhili unaendelea vizuri ujenzi wake na kuleta manufaa kwa jamii, hivyo naomba tuendelee kushirikiana kwa pamoja katika kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo”, alisema Dkt. Ansgar.


Awali akisoma taarifa ya uzinduzi wa mradi huo mbele ya mgeni rasmi Mkurugenzi huyo wa Hospitali ya Misheni Peramiho Dkt. Ansgar, Afisa mtendaji wa kijiji cha Serekano katika kata ya Liganga wilayani Songea, Rehema Nombo alisema kuwa kufanikiwa kwa mradi huo kumetokana na mfadhili huyo kushirikiana pamoja na nguvu za wananchi.

Nombo alifafanua kuwa wananchi wa kijiji cha Liganga wameweza kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya ujenzi huo wa maji kwa nguvu zao wenyewe ikiwemo uchimbaji na ufukiaji wa mitaro na ufukiaji wa mawe, kuchimba na kupakia mchanga, kuchimba eneo la ujenzi wa tanki, kununua mbao kwa ajili ya ujenzi wa tanki hilo, ujenzi wa chanzo cha maji na malipo ya fundi kwa gharama ya shilingi milioni 60.7 ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 85.

Afisa mtendaji huyo aliongeza kuwa kata ya Liganga tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1990 tayari imeweza kupokea miradi mbalimbali ya maendeleo inayohusiana pia na huduma za afya ya msingi ikiwemo mradi wa visima vya jadi, elimu ya afya kwa jamii kupitia Hospitali ya Misheni Peramiho, mafunzo kwa (WAV) yaani Wahudumu wa Afya Vijijini pamoja na elimu ya utengenezaji wa majiko sanifu.

Aliitaja miradi mingine waliyonufaika nayo kuwa ni uboreshaji wa usafi wa mazingira, uhamasishaji wa chanjo  kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na akina mama wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 45, mpango wa afya mashuleni, huduma kwa wagonjwa majumbani, ukarabati wa majengo kama vile zahanati na nyumba ya kuishi mganga.

Kadhalika aliongeza kuwa mpango huo wa huduma ya afya ya msingi umefanikisha kwa kiwango kikubwa kulinda afya za jamii kwa kupunguza na kutokomeza baadhi ya magonjwa na kuifanya jamii ifurahie maisha yenye afya bora.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kata ya Liganga inakabiliwa na changamoto ya kukua kwa kijiji na kuongezeka kwa vijiji vingine pamoja na vitongoji vipya hali ambayo inasababisha maeneo hayo kutofikiwa na mradi huo wa maji.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Songea, Dkt. Yesaya Mwasubira akizungumza katika hafla hiyo fupi ya uzinduzi huo wa mradi wa maji alimpongeza na kumshukuru Dkt. Ansgar kwa mchango wake mkubwa wa kuchangia shughuli za maendeleo kwenye halmashauri hiyo.


Uzinduzi huo wa mradi wa maji ya mtiririko katika kijiji cha Liganga wilayani Songea mkoani Ruvuma, ulikwenda sambamba na utoaji wa zawadi  mbalimbali ikiwemo baiskeli na vyeti kwa Wahudumu wa afya vijijini ambao walijitolea kutoa huduma husika vijijini kwa wananchi na kunusuru maisha ya wagonjwa.

No comments: