Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
DIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mhongozi, Emeran Cyprian
Mapunda (54) katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma amefariki
dunia katika Hospitali ya Misheni Peramiho iliyopo mkoani humo, ambako alikuwa
akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya hiyo, Ambrose Nchimbi alimweleza mwandishi wetu kuwa diwani
huyo amefikwa na mauti usiku wa Juni 23 mwaka huu wakati alipokuwa katika
hospitali hiyo.
Nchimbi alifafanua kuwa kufariki kwa diwani Mapunda kumesababishwa
na tukio la kuanguka Juni 22 mwaka huu akiwa amepanda juu ya mti, wakati
alipokuwa akisafisha shamba lake la kahawa katika kijiji cha Mhongozi kilichopo
kwenye kata hiyo.
“Katika mashamba yetu ya kahawa tumekuwa na tabia ya kupanda
miti ya kivuli, hivyo alikuwa akikata matawi katika miti iliyopo kwenye shamba lake
la kahawa ndipo alipokuwa akishuka kutoka kwenye mti huo kwa bahati mbaya
alianguka akiwa ametanguliza kichwa”, alisema Nchimbi.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Madaktari wa hospitali hiyo wamethibitisha
kifo hicho wakisema kuwa, kimetokana na kuanguka kwake ambako kulisababisha
mshipa mkuu wa mgongoni kupishana na kupoteza mawasiliano na mishipa ya fahamu
iliyopo kichwani.
Alisema kuwa wakati halmashauri hiyo ilipokuwa inafanya utaratibu
wa kumsafirisha kwa njia ya ndege kwenda hospitali ya taifa Muhimbili, ndipo
majira hayo ya usiku alifariki dunia.
Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga,
Christantus Mbunda alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi alisema kuwa chama
hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa kufariki kwa diwani huyo.
“Sisi kama chama limetushitua tukio hili kupoteza kada wetu
ndani ya chama, kata na wananchi aliokuwa akiwaongoza lakini yote haya ni
mapenzi ya Mwenyezi Mungu”, alisema Mbunda.
Pamoja na mambo mengine, marehemu Mapunda ameacha mke na familia ya watoto sita na kwamba mazishi yake yatafanyika Juni 25 mwaka huu majira ya saa saba mchana katika makaburi ya kijiji cha Mhongozi kata ya Mhongozi wilayani Mbinga.
No comments:
Post a Comment