Zeno Mbunda, Diwani kata ya Kitanda Halmashauri ya Mji wa Mbinga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
DIWANI wa kata ya Kitanda kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Zeno Mbunda
amejikuta akiwa katika wakati mgumu baada ya Wajumbe wa Baraza la maendeleo la
kata hiyo, kumkataa wakimtuhumu kufanya ubadhirifu wa mali na fedha za umma.
Aidha Wajumbe hao wamemtaka Diwani wao Mbunda, akae pembeni
kwa kuachia madaraka aliyonayo kutokana na sababu alizosababisha wananchi hao
wakose imani naye na kusababisha kupungua kwa moyo wa kufanya shughuli za
maendeleo ndani ya kata.
Hatua ya Wajumbe wa baraza hilo kumkataa diwani huyo
imefuatia baada ya kutoa malalamiko yao kwa kuandika barua kwenda Ofisi ya Mkuu
wa wilaya ya Mbinga, wakimtuhumu kufanya ubadhirifu huo wa mali za wananchi
wake.
Barua hiyo ya malalamiko iliyoandikwa Mei 25 mwaka huu ambayo
nakala yake tunayo ikiwa na majina na sahihi za mahudhurio ya Wajumbe hao,
wameiomba serikali ichukue hatua dhidi ya kiongozi huyo kwa lengo la kuweza
kunusuru maendeleo ya wananchi wa kata hiyo.
Sehemu ya barua hiyo inasema kuwa kutokana na kikao cha
baraza hilo la kata ya Kitanda kilichofanyika kwa pamoja, walikubaliana
kutomuamini tena na kumkataa kwa sababu ya kupokea mipira (Roll) kumi ya maji
kutoka kwenye mfuko wa Jimbo la Mbinga mjini na kutowasilisha kwa wananchi wa
kitongoji cha Matengo kijiji cha Masimeli kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.
Pia wanamtuhumu kufanya upotevu wa vifaa vya ujenzi ambavyo
ni saruji, nondo na bati za kuezekea baadhi ya majengo katika shule ya
Sekondari Ngwilizi iliyopo katika kata hiyo, vifaa ambavyo vilitolewa na mfuko
huo wa jimbo kupitia usimamizi wake na kusababisha vifaa hivyo kupelekwa
shuleni hapo vikiwa pungufu.
Kadhalika wanadai kwamba alipokea msaada wa fedha taslimu
shilingi milioni 2 toka kwa Shirika la Masista wa Chipole lililopo wilayani
hapa na kutozifikisha kwa Kamati ya ujenzi ya shule hiyo ya Sekondari ili ziweze
kusaidia katika kazi ya ujenzi.
Vilevile wanadai kuwa diwani huyo wa CCM ameshiriki kukusanya
kahawa ya wakulima kupitia kikundi cha Mjimwema kilichopo kwenye kijiji hicho
cha Masimeli, msimu wa mavuno ya zao hilo mwaka 2016/2017 na kutowapa malipo
yao wakulima hao baada ya kuiuza kahawa hiyo ambayo ni zaidi ya tani kumi.
Katika barua hiyo walidai pia kutokana na diwani wa kata ya
Kitanda, Mbunda kutowaheshimu na kutoa dharau kwa viongozi wenzake na watendaji
wa kata hiyo ni kitendo ambacho viongozi hao kinawakatisha tamaa na kukosekana
kwa mafanikio katika maendeleo ya kata.
Pamoja na mambo mengine, diwani huyo wa Chama Cha Mapinduzi
alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo alikataa kuzungumzia lolote
huku akiongeza kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote.
Hata hivyo alipoulizwa Kaimu Mkuu wa wilaya ya Mbinga,
Isabela Chilumba alikiri uwepo wa madai hayo ya wananchi juu ya kumkataa diwani
wa kata hiyo huku akimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba, hawezi kutolea
ufafanuzi wa kina juu ya jambo hilo mpaka atakapowasili Mkuu wa wilaya hiyo,
Cosmas Nshenye ambaye yupo likizo kwenye mapumziko ya kikazi.
No comments:
Post a Comment