Na Julius Konala,
Songea.
KAYA maskini 615 ambazo zimeibuliwa kupitia Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu katika Halmashauri ya Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma, wanatarajia kunufaika na utaratibu mpya uliowekwa na Serikali
namna ya kupokea ruzuku zao kwa njia ya mfumo wa Kielektroniki, mapema mwezi
Julai mwaka huu.
Aniceth Kyaruzi ambaye ni Afisa ufuatiliaji wa mfuko huo
katika Manispaa hiyo, alisema kuwa utaratibu huo mpya utaanza kwa majaribio kwa
kaya ambazo zitakuwa tayari kujiunga na mfumo huo.
Kyaruzi alisema kuwa Manispaa ya Songea ina jumla ya walengwa
4,968 ambapo kati ya hao waliojitokeza mpaka sasa kujiunga na utaratibu huo wa
malipo kwa njia ya Kielektroniki ni 615 wanatoka katika mitaa 53 iliyopo mjini
hapa ambayo utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini umekuwa ukifanyika.
Idadi hiyo ya walengwa alieleza kuwa ni sawa na asilimia 12
ya walengwa wote waliopo na kwamba kigezo kikubwa kinachozingatiwa ni mlengwa
wa mfuko wa TASAF anapaswa kumiliki simu au akaunti ya benki, ambayo atakuwa
akitumia kupokea fedha za ruzuku.
Alifafanua kuwa kaya 4,353 hazikuweza kujiunga na mfumo huo kutokana
na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumia simu ambazo hazikusajiliwa kwa majina
yao, kumiliki simu walizopewa na ndugu zao pamoja na kutojua kusoma na
kuandika.
Kyaruzi aliitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wazee
wenye umri mkubwa kushindwa kumudu kwenda sambamba na utaratibu huo mpya ambao
utaweza kuwalipa fedha hizo kwa
njia ya mfumo wa Kielektroniki.
Pia Afisa ufuatiliaji huyo aliongeza kuwa pamoja na walengwa
wachache kujitokeza katika kuitikia wito wa kukubali mabadiliko ya malipo hayo kwa
njia ya mfumo huo, tayari walengwa wapatao 356 walitoa ahadi ya kununua simu au
kufungua akaunti benki ili waweze kunufaika na utaratibu huo ambao utawapunguzia
adha ya kubeba fedha taslimu wakati wa kwenda kulipa katika kaya maskini.
No comments:
Post a Comment