Na Mwandishi maalum,
Chato.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka maafisa wa Mamlaka ya Mapato hapa
nchini (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasiwatoze kodi
ya majengo Wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.
Alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa akizungumza na wananchi na
viongozi wa wilaya ya Chato mkoa wa Geita ambao walihudhuria uzinduzi wa jengo
la Mamlaka ya mapato wilayani humo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
“TRA ijipange upya namna ya kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai
Mosi mwaka huu, katika kutekeleza jukumu hili zingatieni sheria na taratibu
husika zilizowekwa tusisikie mnawadai kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya
miaka 60 kwa majengo ambayo wanayatumia kama makazi yao,” alisisitiza Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka pia maafisa hao wakusanye kodi ya
majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu.
“Msiende vijijini ambako kuna nyumba za nyasi au za tembe hazihusiki
tembeleeni nyumba za mijini, piteni kwenye mitaa muainishe aina zote za nyumba
zinazostahili kulipiwa kodi mkishafanya sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha
wananchi kulipia kodi hizo”, alisema.
Pia aliwataka wananchi wanaonunua bidhaa wanapaswa kudai risiti mara
wanunuapo bidhaa hizo, lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi
walicholipia.
Vilevile awali akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja
la TRA mkoani humo Kamishna mkuu wa TRA, Charles Kicheere alisema ujenzi huo
ulianza Julai 12 mwaka jana na kukamilika ujenzi wake Juni 12 mwaka huu.
Kicheere aliongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu shilingi bilioni
1.4 na kwamba ulichochewa na ongezeko kubwa la idadi ya walipakodi wilayani
Chato kutoka watu 150 mwaka 2010 hadi 2011 na kufikia watu 600 mwaka jana na
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment