Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
VITENDO vinavyofanywa na baadhi ya Wananchi waishio
katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma vya kufua nguo zao na kuosha Pikipiki
kandokando ya ziwa Nyasa wilayani humo, vimemchukiza Mkuu wa mkoa huo Dkt.
Binilith Mahenge na kufikia hatua ya kupiga marufuku visiendelee kufanyika ikiwa
ni hatua nzuri itakayoweza kudhibiti upotevu wa viumbe hai yakiwemo mazalia ya
samaki yaliyopo kwenye ziwa hilo.
Mkuu huyo wa mkoa amepiga marufuku juzi wakati
alipokuwa wilayani humo akiongoza na kukagua zoezi la kazi ya kufanya usafi
wa mazingira eneo la kijiji cha Mbamba bay, huku akiutaka uongozi wa
wilaya hiyo kuweka utaratibu wa kuzuia vitendo hivyo visiweze kuendelea
kufanyika.
“Sikatazi watu kutumia maji ya ziwa hili kwa ajili ya
shughuli zao za kila siku isipokuwa ninachokataza hapa, watu wasiende hadi
ziwani kufanya shughuli za kufua nguo na kuosha vyombo vyao vya moto badala yake
tumieni maji haya kwa kuyachota kwenye chombo maalum na kwenda kuosha hizi nguo
zenu mbali na ziwa hili”, alisisitiza Dkt. Mahenge.
Alisema kuwa kwenye vyombo vya moto kama vile Pikipiki
kumekuwa na mafuta ambayo ni hatari kwa usalama wa viumbe hai vinavyoishi
kwenye ziwa hilo huku akiongeza kwa kuwataka waache mara moja tabia hiyo ya
kuharibu mazingira ya ziwa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Kufuatia hali hiyo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Nyasa,
Isabela Chilumba kuivunja Kamati ya usimamizi wa mazingira (BMU) wilayani humo
kutokana na kukaidi na kushindwa kutekeleza maagizo ya serikali yanayowataka kusimamia
na kushiriki kikamilifu zoezi hilo la usafi kila mwishoni mwa mwezi.
Alisema kuwa Kamati hiyo haipaswi kuendelea kuwepo
ikifanya kazi ndani ya wilaya hiyo, kwani imeshindwa kutekeleza majukumu
yake yakiwemo kuwachukulia hatua baadhi ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya
uharibifu wa mazingira unaotishia uhai wa viumbe hivyo ndani ya ziwa Nyasa.
Dkt. Mahenge aliagiza pia kwa kuitaka halmashauri ya
wilaya hiyo kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununulia vifaa vya kufanyia usafi
wa mazingira, ikiwemo magari ya kuzolea taka kwani ni aibu kuona wilaya hiyo
haina hata gari moja la kubebea taka au kuwa na kifaa cha kufanyia shughuli za
usafi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Chilumba alimweleza
Mkuu huyo wa mkoa kwamba wilaya itaendelea kusimamia na kutekeleza shughuli
mbalimbali za usafi wa mazingira katika maeneo yote, hata hivyo changamoto
kubwa ni kwa baadhi ya wananchi kutoshiriki kikamilifu katika zoezi
hilo.
No comments:
Post a Comment