Sunday, June 25, 2017

SUPER FEO YAUA TENA SONGEA NA ABIRIA KUJERUHIWA VIBAYA


Na Mwandishi wetu,    
Songea.

HASSAN Ngonyani (25) mkazi wa kijiji cha Likalangiro wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ambaye ni Kondakta wa basi la Kampuni ya Super Feo amefariki dunia, huku baadhi ya abiria waliopanda gari hilo nao wamejeruhiwa vibaya baada ya kupata ajali katika eneo la Hanga Ngadinda halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani humo.

Basi hilo ambalo lilikuwa limebeba zaidi ya abiria 40 likitokea Mbeya kwenda Songea mjini, kati ya hao abiria wanne ndiyo waliojeruhiwa vibaya.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gemin Mushi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 24 mwaka huu majira ya mchana katika eneo hilo, ambapo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Winde Philipo (16) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari ya wasichana Manyunyu iliyopo wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe.

Majeruhi wengine ni Davison Hossea (29) mkazi wa Mbeya, Oddo Bilauli (36) mkazi wa Songea mjini na Engilabeth Mbilinyi (32) mkazi wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Kamanda Mushi alieleza kuwa katika ajali hiyo majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa Songea ambapo wamelazwa wakiwa chini ya uangalizi wa Madaktari.


Alisema kuwa siku ya tukio hilo basi aina ya Higer lenye namba za usajili T 669 DEE la Kampuni ya Super Feo, likiwa kwenye mwendo kasi liliacha njia na kupinduka katika eneo hilo la Hanga Ngadinda.

Kadhalika Kamanda huyo wa Polisi mkoani Ruvuma amewataka waendesha pikipiki maarufu kwa jina la boda boda na madereva wa magari ya abiria kuwa waangalifu pale wanapotumia vyombo hivyo, ambapo Jeshi hilo limejipanga kunyanganya leseni zao kwa wale watakaobainika kukiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo madereva wanaosababisha ajali kwa uzembe.

Hili ni tukio la pili baada ya lingine kutokea Juni 22 mwaka huu likihusisha dereva mmoja wa kampuni hiyo, Ismail Nyami (38) mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea mkoani hapa kufariki dunia papo hapo baada ya basi alilokuwa akiendesha lenye namba za usajili T 213 BNU aina ya Yutong, kugongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T 159 CEX aina ya Iveco Stralis likiwa na tela lenye namba za usajili T 206 CHS mali ya Kampuni ya Trank Link Limited ya Jijini Dar es Salaam na kusababisha abiria kumi na moja kujeruhiwa vibaya.


No comments: