Saturday, June 17, 2017

MLEMAVU WA MIGUU APEWA MSAADA WA BAISKELI NA MBUNGE WA JIMBO LA MBINGA MJINI

Baadhi ya wananchi wa kata ya Mbinga mjini jana wakishuhudia tukio la kukabidhi baiskeli maalumu (Wheel chair) kwa mtoto mwenye ulemavu wa miguu, Batazari Ndunguru ambayo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Sixtus Mapunda.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Geddy Ndimbo naye akijaribu kumwendesha mtoto mlemavu Batazari Ndunguru ambaye ameketi kwenye baiskeli maalumu (Wheel chair) ambayo amepewa msaada na Mbunge wa jimbo hilo.
Mwenyekiti wa kata ya Mbinga mjini, Kalistus Mwamanga akimwendesha mlemavu Batazari Ndunguru ambaye amekaa kwenye baiskeli maalumu (Wheel chair) ambayo amepewa msaada na Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda. (Picha zote na Gwiji la Matukio Ruvuma)
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

BATAZARI Ndunguru (17) ambaye ni mlemavu wa miguu mkazi wa kata ya Mbinga mjini A Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, amepewa msaada wa baiskeli maalumu ya kutembelea (Wheel chair) kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda.

Akikabidhi msaada huo mbele ya uongozi wa kata hiyo kwa niaba ya Mbunge huyo, Geddy Ndimbo ambaye ni Katibu wa Mbunge Mapunda alisema kuwa baiskeli hiyo ya kutembelea mtoto huyo imepatikana kwa thamani ya shilingi 500,000 kutokana na jitihada zilizofanywa na Mbunge wa jimbo hilo.

Ndimbo alisema kuwa jitihada hizo zimefanywa kwa lengo la kumsaidia mtoto huyo ili aweze kuondokana na taabu alizokuwa akizipata kwa siku nyingi, ikiwemo kutambaa kwa mikono na magoti, hivyo aliona kuna kila sababu ya kumtafutia chombo hicho ili kuweza kumrahisishia kutembea vizuri na asiweze kuendelea kupata mateso kama hayo.

“Baiskeli hii nakukabidhi ili iweze kukusaidia na kukurahisishia kutembea vizuri, nawaomba ndugu mnaomtunza endeleeni kuitunza na kumtunza vizuri mtoto huyu kama walivyo wenzake ambao hawana matatizo ya ulemavu, baiskeli itunzwe vizuri itumike kwa matumizi yaliyokusudiwa itakuwa ni ajabu kuona anaitumia mtoto mwingine ambaye hana matatizo ya ulemavu”, alisema Ndimbo.


Kadhalika alitoa rai kwa wananchi wa kata hiyo kwamba ni muhimu sasa wayatambue makundi maalumu kwa kuyajali na sio kuwatenga au kubagua kwa namna moja au nyingine.

Vilevile kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Walemavu (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoani Ruvuma, Martin Mbawala alikemea pia tabia ya wazazi wasiwe wanawafanyia vitendo vya ukatili watoto wenye ulemavu kama vile kuwafungia ndani kwani kufanya hivyo ni kuwanyima fursa muhimu ambazo wanapaswa kuzipata.

“Tusiwe tunawatenga hawa wenzetu, wazazi endapo tutakuwa tukifanya hivi tutakuwa tunakosea hivyo tuwajali kwa kuwapatia haki sawa kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana ulemavu tuache kuwanyanyapaa”, alisisitiza Mbawala.

Pia kwa upande wake akitoa shukrani baada ya kupokea msaada huo mzazi wa mtoto huyo, Analis Hyera alisema kuwa anamshukuru Mbunge huyo kwa kumpatia baiskeli ya kutembelea mtoto wake ambapo alisema itakuwa ni mkombozi mkubwa kwani awali alikuwa akipata shida namna ya kutembea hasa nyakati za masika pale mvua zinaponyesha.

Alieleza kuwa wakati huo wa mvua walikuwa wakilazimika muda mwingi kumbeba mtoto huyo hivyo baada ya kupata baiskeli hiyo sasa ataweza kutembea vizuri bila kupata usumbufu wa aina yoyote ile.

Hata hivyo Diwani wa kata ya Mbinga mjini A, Aurelia Ntani naye akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake wa kata hiyo ambao walikuwa wamewasili wakati wa tukio hilo alitoa shukrani kwa Mbunge Mapunda kwa kuona umuhimu wa kumsaidia mtoto huyo, huku akiongeza kuwa msaada kama huo uendelee kutolewa kwa walemavu wengine pale inapojitokeza fursa ya upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kusaidia watu wenye ulemavu.

No comments: