Na Mwandishi wetu,
Songea.
MASHINDANO Umoja wa Michezo na Sanaa Shule za Sekondari
Tanzania (UMISSETA) kwa mwaka huu, yamefunguliwa rasmi katika mkoa wa Ruvuma kwenye
viwanja vya michezo katika chuo cha ualimu Songea mkoani humo.
Ufunguzi huo ulifanywa juzi na Ofisa elimu wa mkoa huo, Gharama
Kinderu kwa niaba ya Katibu tawala mkoa ambapo aliwapongeza washiriki wote waliotoka
katika wilaya tano za mkoa huo kwa jitihada zao walizofanya katika kushiriki
kikamilifu mashindano hayo.
Kinderu aliwaasa walimu na wanamichezo wote kwa ujumla kuwa
na nidhamu na utii wakati wanapokuwa katika mashindano hayo na kwamba ufunguzi
wa mashindano hayo utawezesha kupatikana timu ya mkoa wa Ruvuma baada ya mchujo
wa vijana kufanyika toka katika kila wilaya.
“Michezo inahitaji nidhamu na jitihada ili uweze kushinda ni
jukumu la walimu kuhakikisha mnasimamia nidhamu ya wanafunzi hawa ili waweze
kupata ushindi na kuleta sifa nzuri katika mkoa wetu”, alisema Kinderu.
Awali akitoa taarifa ya UMISSETA Mratibu wa mashindano hayo, Yovin
Mapunda alieleza kuwa jumla ya wanamichezo 420 na walimu 56 toka wilaya tano za
mkoa huo, wamekutana kwa lengo la kuunda timu ya mkoa itakayokwenda kushiriki
mashindano ya taifa mkoani Mwanza mwezi Juni mwaka huu.
Aliongeza kuwa kati ya wanamichezo hao wavulana ni 265 na
wasichana 196 ambao watashindana katika michezo tisa ili kupata timu ya mkoa
kuanzia Mei 28 hadi 30 mwaka huu.
Mapunda aliitaja michezo inayoshindaniwa kuwa ni soka
wavulana, soka wasichana, netiboli, mpira wa mikono, mpira wa wavu, riadha
wavulana, riadha wasichana, mpira wa kikapu, mpira wa meza na bao.
Kwa mujibu wa ratiba timu ya mkoa itakayoundwa itakaa kambini
kuanzia Mei 31 hadi Juni 03 mwaka huu na kwamba itaelekea Mwanza kwa ajili ya
kufanya mashindano ya UMISSETA Taifa.
Kinderu alionya pia dhidi ya vitendo vibaya vya upendeleo
vinavyoweza kufanywa na walimu akitaka viachwe mara moja visifanyike, ili vijana
hao waweze kwenda kushiriki michezo hiyo wakiwa na sifa nzuri ambapo atakayebainika
kujihusisha na njama zozote za kuzorotesha timu ya mkoa hatua kali za kinidhamu
zitachukuliwa.
Pamoja na mambo mengine Washiriki hao wote wa mashindano hayo wanatoka katika
wilaya tano za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na
Tunduru.
No comments:
Post a Comment