Na Muhidin Amri,
Madaba.
WAKULIMA katika Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma
wametakiwa kuchangamkia fursa na mkakati uliowekwa na serikali ambao unataka
nchi kufikia katika uchumi wa kati, kupitia ujenzi wa viwanda vya aina
mbalimbali ifikapo mwaka 2020 hadi 2025.
Shafi Mpenda. |
Vilevile katika kufanikisha hilo imeelezwa kuwa wanapaswa
kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani ili viwanda hivyo vitakapoanzishwa, viweze
kusonga mbele na kusaidia kuongeza thamani ya ubora wa mazao hayo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Shafi
Mpenda alisema hayo juzi wakati alipokuwa akikagua mradi wa shamba la mahindi
la vijana, ambao hujishughulisha pia na uendeshaji wa Pikipiki maarufu kwa jina
la Boda boda katika kijiji cha Lutukira wilayani humo ili waweze kujipatia
kipato.
Alisema kuwa wilaya ya Madaba ni maarufu kwa uzalishaji wa
mazao ya chakula na biashara kutokana na uwepo wa hali nzuri ya hewa, lakini
bado wananchi wake wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na mazao
wanayolima hayawanufaishi ipasavyo kwa sababu ya ukosefu wa soko la kuuzia
mazao hayo na viwanda vya kusindika ambavyo vingewawezesha kuongeza thamani ya
mazao yao.
Mpenda aliongeza kuwa wakulima hao licha ya juhudi kubwa
wanazozifanya mwaka hadi mwaka katika kuzalisha mazao ya tangawizi, matunda ya
aina mbalimbali, mahindi na mpunga bado changamoto wanayokabiliana nayo ni soko
la uhakika na viwanda vitakavyoweza kuongeza thamani ya mazao hayo
wanayozalisha.
“Halmashauri hii ya Madaba ina utajiri mkubwa wa ardhi na
rasilimali watu na kwamba tutaweza kupiga hatua mbele kiuchumi endapo tu wananchi
hawa hasa kwa upande wa wakulima, wataweza kubadili mfumo kutoka kilimo
cha mazoea (zamani) na kuingia katika mfumo wa kisasa kwa kutumia kilimo
cha Trekta na kuweka shambani pembejeo bora za kisasa kipindi cha upandaji wa
mazao yao”, alisema.
No comments:
Post a Comment