Na Mwandishi wetu,
Songea.
JITIHADA zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Magufuli katika kudhibiti vitendo vya wizi wa rasilimali za
nchi yakiwemo madini, zimepongezwa na baadhi ya Wananchi wa Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
wa kata ya Mateka katika Manispaa hiyo, Kazira Hussein.
Rais Dkt. John Magufuli. |
Wananchi hao kwa nyakati tofauti walisema kuwa kitendo cha
Rais Dkt. Magufuli kubaini mbinu chafu zilizokuwa zinafanywa na viongozi ambao
siyo waaminifu, ambao walikuwa wakiidanganya serikali kwamba wanasafirisha
mchanga usiokuwa na madini na kuupeleka nje ya nchi, wakati mchanga huo ulikuwa
na madini ni jambo ambalo linasikitisha na kudhihirisha kuwa kwa muda mrefu
Watanzania walikuwa wanaibiwa.
Joseph Milanzi mkazi wa Lizaboni alieleza kuwa kazi
inayoendelea kufanywa na Rais huyo katika kuwabaini wahalifu hao, inapaswa kuungwa
mkono kwa nguvu zote ili kuweza kulifanya taifa liweze kukua kiuchumi kupitia
rasilimali zake na sio muda mwingi kutegemea misaada kutoka nje ya nchi.
Kazira Hussein ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Mateka
iliyopo mjini hapa alisema kuwa sifa ya Rais Dkt. Magufuli inazidi kukonga
mioyo ya Watanzania wengi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa na uchungu kutokana na
wizi huo wa madini na mikataba mibovu iliyokuwepo ambayo ilisababisha wizi huo
uendelee kufanyika.
Alisema kuwa kufuatia hali hiyo wananchi wengi walikuwa
wakishindwa kupata huduma za msingi kama vile afya, kilimo na elimu ikiwemo
kupunguza makali ya maisha ambayo wamekuwa wakiendelea kupambana nayo hadi sasa.
Kadhalika Herman Komba mkazi wa Msamala naye aliongeza kuwa
kiongozi huyo Watanzania hawakukosea kumchagua kwani ameonesha msimamo wa hali
ya juu ambao hata wananchi na wanasiasa wengine wamekuwa mstari wa mbele
kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika kupigania haki ya wananchi wake.
Pamoja na mambo mengine wananchi hao wa Manispaa ya Songea walisema
kuwa kuna kila sababu kwa Watanzania kuona umuhimu wa kufanya maandamano ya
amani nchi nzima, ambayo yatalenga kumpongeza Rais Dkt. Magufuri na kuzungumzia
mstakabali mzima wa uchumi wa nchi yetu huku wakiliomba hata Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kufanya kazi kwa makini hasa pale wanapojadili na
kupitisha mikataba yenye maslahi na taifa hili.
No comments:
Post a Comment