Ziwa Nyasa. |
Na Muhidin Amri,
Nyasa.
HALMASHAURI wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, imeanza
kazi ya ujenzi wa barabara zake za mitaa kwa kiwango cha changarawe ikiwa ni
mpango wa kuboresha barabara hizo, ili ziweze kuwa katika hali nzuri na
kurahisisha kukua kwa maendeleo katika wilaya hiyo hususan usafirishaji mazao
kutoka shambani hadi sokoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Oscar Mbyuzi
alisema hayo juzi wakati wa zoezi la ufunguzi rasmi ujenzi wa barabara hizo
zenye urefu wa kilometa nane katika kijiji cha Kilosa wilayani hapa.
Dkt. Mbyuzi alisema kuwa mradi huo ulianza tangu mwezi
Februari mwaka huu na kwamba utakuwa endelevu kila halmashauri yake itakapokuwa
na fedha za kutosha kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.
Wilaya ya Nyasa ina jumla ya kilometa 45 za barabara
za mitaa ambazo zimeainishwa kisheria na kupimwa katika mpango wa mipango miji
ambapo wilaya hiyo, imejiwekea mikakati ya kuboresha barabara zake kutoka
kiwango cha udongo hadi changarawe kilometa tano kwa kila mwaka ili ziweze kuwa
bora zaidi na kufanya zipitike kwa kipindi chote cha mwaka.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mradi
wa barabara kilometa nane za mitaa hadi sasa umegharimu jumla ya shilingi
milioni 170,235,897 ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu shilingi 161,164,636 na
mchango wa halmashauri ni shilingi 9,071,261.
Aidha alisema kuwa licha ya barabara hizo kujengwa kwa
kiwango hicho zitasaidia pia kuimarisha maendeleo ya vijiji vitakavyopitiwa na
mpango huo kuwa na muonekano mzuri, sambamba na kuvutia watalii watakao kuwa
wakienda wilayani humo kwa ajili ya shughuli za utalii.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo na
mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kutumia fursa zilizopo ndani ya mkoa huo, kwa ajili
ya kuwekeza miradi mbalimbali ya kiuchumi wilayani Nyasa kama vile ujenzi
wa hoteli za kisasa kwani kufanya hivyo kutasaidia uwepo wa ongezeko kubwa la
watalii wanaotoka ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment