Na Muhidin Amri,
Songea.
JUMLA ya shilingi milioni 65.710 zimetumika kwa ajili
ya ujenzi wa kisima cha maji katika kijiji cha Lundusi kata ya Maposeni,
Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ikiwa ni malengo ya kufikisha
huduma ya maji safi na salama katika makazi ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya kijiji hicho.
Mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo Isaac Nyirenda
alisema kuwa mbali na wananchi hao kufikishiwa katika makazi yao pia maji hayo yatapelekwa
makao makuu ya halmashauri pamoja na nyumba ya kuishi Mkurugenzi mtendaji na
watumishi wengine wa halmashauri.
Alisema kuwa mpango wa baadaye ni kuhakikisha kwamba
huduma hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi ambao wanaishi katika maeneo
mbalimbali ya kata yote ya Maposeni na kata nyingine za jirani.
Kwa mujibu wa Mhandisi huyo alifafanua kuwa kazi zote
za ujenzi huo wa kisima zimefanywa kwa kutumia mafundi na wataalamu wa halmashauri
kwa kushirikiana na mafundi wadogo ambao waliingia nao mikataba.
Nyirenda alieleza kuwa hadi sasa kazi iliyofanyika ni
uchimbaji visima vitatu na matanki yake ya kuhifadhia maji, ujenzi wa nyumba ya
kuishi mlinzi pamoja na uzio, uchimbaji wa choo na mtaro kilometa 1.145, ununuzi
wa mabomba na viunganishi vyake pamoja na ununuzi wa pampu tatu za kuvuta maji.
Alibainisha kuwa Pampu iliyofungwa katika kisima hicho
ni ya aina ya “Grundfos Pump” yenye uwezo wa nguvu kiasi cha kilowati 1.5 ambayo
uwezo wake ni mkubwa wa kusukuma maji kwa mita 150.
Pia kwenye matanki hayo ya hifadhi ya maji itakuwa na
uwezo wa kusukuma maji kwa kiwango cha lita 8,400 kwa saa au lita 140 kwa
dakika na visima hivyo vina ujazo wa mita za ujazo 13.73 ambazo ni sawa na lita
13, 730 kwa wakati mmoja.
No comments:
Post a Comment