Waumini wa Kiislamu kutoka mtaa wa Making’inda Manispaa ya Songea, wakitoka nje baada ya kuswali swala ya Ed el Fitri. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
IKIWA ni siku chache zimepita katika kusherehekea sikukuu ya
Idd el Fitri, Waislamu hapa nchini wametakiwa kujiepusha na mambo yanayokwenda
kinyume na mafundisho ya dini yao, ikiwemo matendo ya uzinzi na tabia
ya kujengeana fitina badala yake wanapaswa kuendelea kutenda
mambo mema waliyokuwa wakiyafanya wakati wa mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
Aidha wameombwa kudumisha upendo, undugu na mshikamano
miongoni mwao na hata kwa watu wasiokuwa Waislamu hatua ambayo itasaidia kuwa
na jamii ya watu wastaarabu ambao wakati wote wataishi na kumcha Mungu.
Imamu wa Msikiti wa Making’inda kata ya Msamala Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma, Shehe Bashiru Yahay Matembo alisema hayo jana wakati
akitoa nasaha kwa waumini wa kiislamu huku akisisitiza kuwa Waislamu wanapaswa
kutumia sikukuu ya Idd el Fitri, kwa ajili ya kusameheana na kuomba msamaha kwa
yule aliyemkosea badala ya kuendeleza chuki na uhasama kati yao.
Alisema kuwa wakati umefika sasa kwa Waislamu pia kuwa kitu
kimoja na kuendeleza utamaduni wa undugu pamoja na kukataa mambo mabaya kwa kuhimizana
kutenda mambo mazuri, kwani kufanya hivyo husaidia kudumisha mshikamano uliokuwepo
hapo awali.
Kwa mujibu wa Shehe Matembo alieleza kuwa kwa waumini wa dini
hiyo kurudia tena kufanya maovu haipendezi na kwamba kumalizika kwa mwezi mtukufu
wa Ramadhani, iwe ndiyo mwanzo wa kuongeza jitihada katika kutenda na
kufuata mambo mema ikiwemo kusoma kitabu kitukufu cha Quran, hatua ambayo itawasaidia
hata katika kufahamu vizuri dini yao pamoja na kuzidisha upendo miongoni mwao.
Pia amewakumbusha wazazi wahakikishe kwamba wanawatunza
na kuwalea watoto wao katika misingi ya dini, ili kuepukana na kizazi
kisichomjua Mungu jambo ambalo ni hatari kwa kuwa jamii isiyomcha Mwenyezi
Mungu ndiyo chanzo cha kuongezeka na kukithiri kwa vitendo vya uzinzi, ulevi na
wizi wa mali za umma.
No comments:
Post a Comment