WAZIRI wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
George Simbachawene amewaonya Wakuu wa mikoa na wilaya, ambao wanatumia vibaya
madaraka yao ya kukamata watu walio kwenye himaya zao.
Alitoa onyo hilo leo wakati alipojibu
maswali ya wabunge waliotaka kufanyika marekebisho ya sheria inayowapa mamlaka
wakuu hao ya kuwakamata na kuwaweka ndani wananchi wanaowatuhumu kwa lolote.
Licha ya kubainisha kwamba sheria
hiyo haina tatizo, Waziri huyo amesisitiza kwamba, ukamataji unatakiwa ufanywe
kwa mtu aliyetenda kosa la jinai au anayehatarisha usalama, “isiwe kwa show-off
tu”, alisema.
Vilevile aliongeza kuwa mhusika anayekamatwa
na kuwekwa ndani anatakiwa kufikishwa Mahakamani mara moja na asishikiliwe tu.
Alisisitiza kuwa wakuu hao wa
mikoa na wilaya ni wawakilishi wa Serikali kwenye maeneo yao, hivyo hawatakiwi
kutumia vibaya madaraka waliyokasimiwa.
Katika siku za hivi karibuni wakuu
wa mikoa na wilaya wamekuwa wakilalamikiwa kuwaweka watu kizuizini pasipo kuwa
na sababu za msingi, miongoni mwao wakiwamo waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment