Na Muhidin Amri,
Mbinga.
WANAWAKE zaidi ya 150 kutoka katika vijiji vitatu kata ya
Kigonsera Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamepata mafunzo ya
ujasirimali na kufanikiwa kujiunga kwenye vikundi vinavyowawezesha kujijenga
kiuchumi kwa lengo la kuboresha maisha yao.
Akizungumza jana wakati wa kufunga mafunzo hayo Diwani
wa viti maalum wa tarafa ya Kigonsera wilayani humo, Amina
Kapinga alieleza kuwa mbali na wanawake hao kunufaika na elimu hiyo ya
ujasirimali pia baadhi yao wameanza kupewa mikopo ya fedha na pembejeo za
kilimo kupitia vikundi hivyo.
Kapinga alifafanua kuwa mikopo na fedha hizo wamepata kutoka
kwenye taasisi mbalimbali na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS).
Alisema kuwa katika kata hiyo tayari vikundi vitatu vya
Mwongozi na Kitumbalomo ambavyo hujishughulisha na shughuli za kilimo na
vingine vinavyotengeneza sabuni na nguo aina ya batiki vimeweza kunufaika na
mikopo hiyo.
Lengo kubwa la wanawake hao kuanzisha na kujiunga katika vikundi
hivyo ni kuweza kupata mikopo ya kuendeshea shughuli zao hususan katika sekta
ya kilimo, kwani mpaka sasa ni asilimia 90 tu ndio ambao hujishughulisha katika
sekta hiyo muhimu.
Diwani huyo alibainisha kuwa shughuli hizo wanazozifanya
huwawezesha pia kupata fedha kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kiuchumi, kusomesha
watoto wao, ujenzi wa nyumba bora na hata kununua vyombo vya usafiri ambavyo
huwasaidia kurahisisha majukumu yao ya kazi za kila siku.
Kapinga alisema, mafunzo hayo kwa wanawake hao yalitolewa
na wataalamu kutoka taasisi za kifedha (Benki) chini ya udhamini wa
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Ruvuma, Kuruthum Mhagama ambayo
yalifanyika mjini Songea mkoani humo.
“Nawaomba hata watu wengine binafsi na taasisi nyingine za
kifedha zijitokeze kuwasaidia hawa wanawake kuwapatia mikopo ya fedha, ili waweze
kuimarisha vikundi vyao kwa sababu ukimsaidia mwanamke umesaidia jamii ya kitanzania
kutokana na umuhimu mkubwa wa mwanamke katika familia”, alisema Kapinga.
Alisema kuwa mwanamke anao mchango mkubwa katika familia
na taifa kwa ujumla kwani ndiye mzalishaji mkubwa ikilinganishwa na mwanaume,
hivyo ni vyema sasa serikali ikaona umuhimu wa kusaidia makundi mbalimbali ya
wanawake ambao wamejiunga pamoja kwenye vikundi vya ujasiriamali katika
kupambana na umaskini.
No comments:
Post a Comment