Na Kassian Nyandindi,
Madaba.
MBIO za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu katika wilaya ya
Madaba mkoani Ruvuma, zimeingia dosari kufuatia kiongozi wa mbio hizo, Amour Hamad
Amour kukataa kuzindua mradi wa Bwalo la chakula shule ya msingi Lilondo
iliyopo katika halmashauri ya wilaya hiyo.
Kukataa kufunguliwa kwa mradi huo kumemfanya Mkuu wa wilaya
hiyo, Pololet Kamando Mgema kujikuta akiwa katika wakati mgumu baada ya Kiongozi
huyo kumbana maswali magumu.
Aidha Amour alisema kuwa taarifa za ujenzi wa mradi huo
alikuwa nazo tokea awali kabla ya kuwasili katika eneo la mradi, hivyo ana wasiwasi
hata jengo hilo huenda likawa limebadilishwa matumizi yake.
“Tutoe mfano, hata kama leo hii Rais wa nchi anakuja
kuufungua mradi huu katika wilaya yako unaweza kumleta katika mradi kama huu”,
? alihoji Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa.
Alisema kuwa hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa miradi mingi
ambayo inaanzishwa katika wilaya ya Madaba, haichukuliwi hatua ya haraka katika
kutoa huduma kwa walengwa.
Kadhalika kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea, Pololet Kamando Mgema
alisikika akisema, “Mimi naomba nikiri mapungufu haya yaliyopo hapa, kwa sababu
sikuwepo wakati mradi huu unajengwa”.
Pia Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, kukataa kufungua
mradi huo alieleza kuwa jengo hilo limejengwa chini ya kiwango ukilinganisha na
thamani halisi ya fedha iliyotumika katika kazi ya ujenzi wake shilingi milioni
19,460,000 huku taarifa za mradi huo nazo zikiwa zinakinzana.
Alieleza kuwa Mwenge wa Uhuru hauwezi kuzindua bwalo hilo
ambalo thamani yake haiendani na kazi iliyofanyika hivyo kutakuwepo na utumiaji
wa fedha ovyo kinyume na utaratibu husika.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa
msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari unathibitisha kuwa jengo hilo liliwekewa
jiwe la msingi na aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu mwaka 2013
ambapo ndiyo ujenzi wake ulianza kufanyika.
No comments:
Post a Comment