Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KIONGOZI Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad
Amour amewataka Watendaji waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma wahakikishe kwamba, fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi zinafanya kazi iliyolengwa ipasavyo
ili ziweze kuleta tija katika jamii.
Aidha ameagiza kwamba miradi hiyo inapaswa kutekelezwa
kwa wakati, ili kuweza kusaidia kuharakisha mipango mbalimbali ya kimaendeleo
ambayo inalenga kuwaondolea umaskini wananchi.
Hayo yalisemwa juzi na kiongozi huyo wa mbio hizo za
Mwenge wa Uhuru wakati alipokuwa katika halmashauri ya mji huo akikagua jumla
ya miradi kumi yenye thamani ya shilingi milioni 435,332,081 ambayo Mwenge huo
umeweza kufanya kazi ya kuweka mawe ya msingi, kufunguliwa, kukaguliwa na
kuzinduliwa.
Katika miradi hiyo amepongeza jitihada zilizofanywa za
utekelezaji wake ambapo nguvu za wananchi zimetumika shilingi milioni
48,598,400 mchango wa halmashauri milioni 6,095,000 serikali kuu milioni
166,176,301 wadau wa maendeleo milioni 20,462,380 na watu binafsi ni shilingi
milioni 194,000,000.
“Ni wajibu wenu watumishi wa umma kufanya kazi kwa
kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa na serikali ili tuweze kufikia malengo
tuliyojiwekea na kulifanya taifa letu liweze kusonga mbele kimaendeleo na
wananchi waweze kuondokana na umaskini”, alisisitiza Amour.
Vilevile aliwataka watendaji hao wa serikali kutenga
maeneo maalumu kwa ajili ya vijana kufanya biashara na shughuli zao mbalimbali
za kimaendeleo ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kukua kiuchumi.
Kadhalika alisisitiza kuwa vijana hao wahamasishwe pia
kuunda vikundi vya ujasiriamali, ambavyo vitasajiliwa kisheria na kuweza
kuwafanya waweze kukopesheka na taasisi za kifedha katika kuendeleza shughuli
zao za ujasiriamali.
Pamoja na mambo mengine, kwa mujibu wa risala ya utii wa
wananchi wa halmashauri ya mji wa Mbinga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Magufuli ambayo ilisomwa na Mkuu wa wilaya hiyo Cosmas
Nshenye alisema kuwa tathmini ya mwaka 2016 inaonesha kuwa pato la mwananchi wa
kawaida kwa mwaka katika halmashauri hiyo linakadiriwa kuwa ni shilingi milioni
1,500,000.
Lengo la Halmashauri hiyo alisema ni kuongeza pato hilo
la sasa na kufikia milioni 2,500,000 ifikapo mwaka 2025 kutokana na wananchi
wengi kuwa na mwitikio mkubwa wa kufanya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo
cha mazao ya chakula na biashara.
Mwenge huo ambao umebeba ujumbe wa kitaifa (Shiriki
kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu) katika halmashauri ya mji
wa Mbinga umeweza kupita kwenye miradi hiyo ambayo ni ya sekta ya
elimu, afya, barabara, maji, kilimo, ufugaji
nyuki, kiwanda cha kusindika unga wa mahindi pamoja na sekta ya
mazingira upandaji miti na ujenzi wa nyumba bora ya kuishi
mwananchi.
Hata hivyo katika risala hiyo Nshenye aliongeza kuwa kwa
upande wa uwezeshaji wa vijana kiuchumi halmashauri katika
mwaka wa fedha 2016/2017 imeweza kutenga asilimia tano ya mapato yake ya
ndani yenye jumla ya shilingi milioni 76,100,000 kwa ajili ya
kuwezesha vijana katika shughuli za kukuza uchumi na kwamba tayari
mpaka sasa imekwisha toa mikopo kwa vikundi vitano vya vijana yenye thamani ya
shilingi milioni 6,000,000 ambavyo vinajishughulisha na kilimo na biashara
mchangayiko.
No comments:
Post a Comment