Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
Mbinga.
SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imechukua hatua ya
kumsimamisha kazi Mhandisi idara ya maji wilayani humo Vivian Mndolwa kwa lengo
la kupisha uchunguzi juu ya ujenzi wa mradi wa maji uliopo katika kitongoji cha
Mnazi mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako, ambao unadaiwa kujengwa chini ya
kiwango na kushindwa kuwafikishia maji wananchi katika maeneo husika ndani ya
kata hiyo.
Vivian Mndolwa. |
Aidha kusimamishwa kazi kwa Mhandisi huyo kunafuatia agizo
lililotolewa Mei 8 mwaka huu na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa,
Amour Hamad Amour wakati anaukagua mradi huo ili Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas
Nshenye aweze kuunda kamati itakayofanya kazi ya kuchunguza tatizo hilo na
baadaye hatua husika ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika waliouhujumu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini
kuwa Mhandisi huyo pia analalamikiwa akidaiwa kushindwa kusimamia kikamilifu taratibu za
ujenzi wa mradi huo wa maji.
Mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 kwa gharama ya
shilingi milioni 718,896,533 chini ya ufadhili wa benki ya dunia ambapo ilibidi
ujenzi wake ukamilike katika kipindi cha mwaka mmoja tangu uanze kujengwa,
lakini hadi kufikia kipindi cha mwaka huu 2017 ujenzi huo bado haujakamilika na
fedha za mradi huo zimetumika katika kazi hiyo ya ujenzi.
Vilevile kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imeelezwa
kuwa ni ya PATTY Interplan ya kutoka jijini Dar es Salaam na kwamba mkandarasi
huyo ananyoshewa kidole kuwa anadaiwa kutokomea kusikojulikana na kuacha
mafundi wake katika eneo la mradi bila kazi ya ujenzi huo kukamilika ipasavyo.
Mpaka sasa hatua ya ujenzi wa mradi huo yamejengwa matenki
mawili ya maji ikiwemo moja kubwa lenye ujazo wa lita 200,000 na lingine ndogo
lenye ujazo wa lita 75,000 na ufukiaji chini wa mabomba ya Plastiki kutoka
kwenye chanzo kikuu cha kuleta maji katika matenki hayo.
Kadhalika vituo 36 vya kuchotea maji vimejengwa lakini
kutokana na ucheleweshaji wa ujenzi wa mradi huo na kuleta maji kwenye mabomba
hayo kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa kata ya Mkako wilayani humo, inadaiwa
kuwa siku kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru alipowasili hapo
walipojaribu kuleta maji kwenye matenki hayo kwa ajili ya kupeleka kwenye vituo
hivyo vya kuchotea maji, mabomba hayo yalikuwa yamepasuka na kushindwa kuleta
maji jambo ambalo linadhihirisha kuwa ujenzi wa mradi huo ni wa chini ya
kiwango.
Hivyo basi, Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga imeunda Kamati
maalumu ya watu saba ambao ni wataalamu watakaoweza kuchunguza tuhuma hizo na
mambo mengine yanayohusiana juu ya mradi huo.
Akizungumza na mwandishi wetu Kaimu Mkuu wa wilaya hiyo,
Gilbert Simya alisema kuwa timu hiyo ya wataalamu ambayo imeundwa kuchunguza
jambo hilo inatoka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, Ofisi ya mkuu huyo wa
wilaya na wengine ni wajumbe wa ngazi ya halmashauri ya wilaya.
Gilbert ambaye pia ni Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga
alithibitisha kwa kusema kuwa kamati hiyo imeanza kufanya kazi rasmi Mei 12
mwaka huu na kwamba itakamilisha majukumu yake katika kipindi kisichozidi siku
kumi.
“Msimamizi mkuu wa ule mradi ni Mhandisi mwenyewe wa maji wa
wilaya, tunafanya kazi ya uchunguzi juu ya historia ya ule mradi namna
ulivyotekelezwa na mwisho wa siku ukweli utakaopatikana kwa namna yoyote ile
tutatoa taarifa ya mradi nini kinaendelea na hatua zipi zimechukuliwa katika
jambo hili”, alisema.
No comments:
Post a Comment