Na Mwandishi wetu,
Songea.
BAADHI ya Wananchi waishio katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameonesha kufurahishwa kwao na huduma za Simbanking ambazo zinatolewa na benki ya CRDB, hivyo kuwawezesha kufanya miamala ya kifedha kupitia simu zao za mkononi pasipo usumbufu wa aina yoyote ile.
Wameeleza kuwa wanaweza kufanya miamala mbalimbali kama vile kuhamisha fedha zao kutoka kwenye akaunti walizonazo katika benki hiyo kwenda kwenye mitandao mingine ya simu na kulipia bili za umeme na mambo mengineyo.
Aidha walisema kuwa huduma hiyo imerahisisha kwa kiwango kikubwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kama vile kununua pembejeo kwa kufanya malipo moja kwa moja kwa kutumia huduma ya Simbanking.
Ibrahim Luanda ambaye ni mkazi wa mtaa wa Luhira, Yona Mkuta wa Miembeni na Elias Fanuel mkazi wa mtaa wa Majengo mjini hapa walisema huduma hiyo kwao imewasaidia kuongeza hata kiwango cha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Walisema kuwa hivi sasa hawalazimiki kutumia gharama za usafiri kwenda benki ya CRDB kufuata huduma ya kutoa fedha kwa ajili ya kufanyia shughuli zao mbalimbali badala yake hutumia mawakala waliopo mtaani kukamilisha miamala yao.
“Huduma hii licha ya kufanikisha katika masuala ya kibenki, pia inatuwezesha hasa kwa wananchi wengi tunaoishi vijijini kuokoa muda wetu wa kufanya shughuli zingine za kimaendeleo na kuamini kwamba hata fedha tunazoweka kwenye akaunti zetu zipo salama”, walisema.
Yona Mkuta naye alisema kuwa tangu ajiunge na huduma ya Simbanking amepata faida lukuki kama vile kurahisisha shughuli zake za kibiashara kwani ameweza kununua bidhaa moja kwa moja bila kutumia utaratibu wa zamani wa kwenda kuchukua fedha benki badala yake anatuma fedha kutoka kwenye akaunti yake hadi kwa wafanyabiashara wengine wenye maduka ya jumla kwa ajili ya kupata bidhaa.
Alisema utaratibu huo pia umesaidia kukomesha vitendo vya wizi kwani siku za nyuma baadhi yao wameshaibiwa kwa kuwa walilazimika kutembea na kiasi kikubwa cha fedha mifukoni kwa ajili ya kununua bidhaa na mahitaji mbalimbali.
Kwa upande wake akizungumzia huduma hiyo Meneja biashara wa benki ya CRDB tawi la Songea, Godfrey Kamugisha alisema, benki hiyo inaendelea kuongeza huduma zake karibu zaidi na wateja wake ili waweze kupata huduma bora zaidi za kibenki kupitia simu zao za mkononi.
Kamugisha aliongeza kuwa wao wanathamini wateja wao hivyo wakati wote wanahitaji kuona wanapata huduma bora kwa kuokoa muda wao ili waweze kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.
Pamoja na mambo mengine amesisitiza kwamba miamala yote inayofanywa kupitia Simbanking kupitia benki hiyo inalindwa na namba ya siri (PIN) inayojulikana na mteja mwenyewe, hivyo amewahakikishia wateja wote kuwa huduma hii ni salama wakati wote wanachopaswa ni kuendelea kutunza namba zao za siri.
No comments:
Post a Comment