Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KUFUATIA kufukuzwa kazi kwa
baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ambrose Nchimbi amewataka watumishi wengine
waliopo katika wilaya hiyo waondokane na tabia ya wizi wa mali za umma na tabia
ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Taswira mpya ni kufanya kazi
kwa misingi ya utawala bora inayotaka serikali hii ya awamu ya tano na sio muda
mwingi kufikiria vitendo viovu ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi
wetu”, alisema.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti
huyo wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya
kuhitimisha juzi kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Nchimbi alitoa rai kwa
watumishi hao kwamba hivi sasa wanapaswa kubadilika na sio kila siku wanakuwa
ni watu ambao wanafanya makosa kwa makusudi huku wakijiua kwamba wanaumiza
wananchi.
Alisisitiza kuwa yeye na
Madiwani wenzake wamefikia hatua ya kuwafukuza kazi watumishi wanne waliobainika
kufanya makosa ya uzembe na ubadhirifu wa mali za umma ili iweze kuwa fundisho
kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
“Madiwani tumefanya hivi
kuweza kutoa fundisho kwa wale wengine waliobaki ili waweze kufanya kazi vizuri
kwa misingi bora na taratibu zilizowekwa na serikali, hatutaki kumuona mtumishi
anakuwa na tabia ya wizi na udanganyifu katika utendaji wake wa kazi za kila
siku za utumishi wa umma”, alisema.
Vilevile aliwataka pia
Madiwani wahakikishe kwamba wajitambue katika nafasi zao walizonazo kwa
kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi kwenye maeneo
yao ili iweze kujengwa kwa viwango vinavyokubalika.
Pamoja na mambo mengine
watumishi waliofukuzwa kazi katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuwa ni
aliyekuwa afisa mtendaji wa kata ya Kitura, Daniel Komba ambaye amefukuzwa kazi
kutokana na kufanya matendo kinyume na dhamira njema ambapo alifoji risiti za
marejesho ya fedha shilingi 350,000 ambazo ni michango ya wananchi wa kata hiyo.
Imebainishwa kuwa fedha hizo
walikuwa wamechanga wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo yao ambapo
alizitafuna kwa manufaa yake binafsi na halmashauri ilipofanya ufuatiliaji wa
kina ilibaini kwamba risiti aliyoitumia kukusanyia fedha hizo haikuwa risiti
halali ya serikali.
Vilevile wengine ni Ramadhan
Mang’una ambaye ni afisa kilimo msaidizi, Allan Ndunguru afisa mtendaji wa
kijiji cha Ulima na Michael Nakitundu naye ni afisa mtendaji wa kijiji cha
Ulolela ambao nao walishiriki kufanya ubadhirifu wa mali za umma katika vijiji
hivyo.
No comments:
Post a Comment