Baadhi ya wananchi wakiondoa paa la nyumba ili kuokoa watu waliokuwa wameangukiwa na mti huo majira ya usiku. |
Miili ikiwa imeshapakiwa ndani ya gari la Polisi kwenda kuhifadhiwa hospitalini. |
Na Mwandishi wetu,
Arusha.
MVUA zinazonyesha mfululizo mkoani Arusha, zimeleta maafa
makubwa katika familia ya mzee Jonathan Kalambiya (55) ambaye ni mkazi wa mtaa
wa Sokoni katika kijiji cha Kinyeresi wilayani Arumeru mkoani humo, baada ya
mti mkubwa uliong’olewa na maji ya mvua hizo kuangukia nyumba yake na kuua
watoto wake watano.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya usiku baada ya mti huo kuangukia
nyumba yake na kuleta madhara hayo.
Charles Mkumbo ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoani Arusha amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuwataja watoto hao waliofariki dunia kuwa ni Miliamu
Jonathan (16) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Inaboishu.
Kamanda huyo alimtaja mwanafunzi mwingine kuwa ni Grolia
Jonathan (11) mwanafunzi wa shule ya msingi Kinyeresi iliyoko wilayani Arumeru
mkoani humo.
Alisema watoto wengine wa mzee huyo kuwa ni pamoja na mtoto
wa kwanza wa mzee huyo aliyetambuliwa kwa jina la Giliad Jonathan (31), Lazaro
Lomnyaki (26) na Best Jonathan (20).
Kamanda Mkumbo alisema kuwa mti huo uliangukia nyumba hiyo
baada ya kung’olewa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mfululizo katika Jiji hilo
la Arusha.
Pia amewataka wakazi wa Arusha kuchukua tahadhari katika
kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, kwa kukarabati nyumba zao
na kuacha kujenga chini ya miti ama kwenye vyanzo vya maji.
Alisema kujenga katika vyanzo vya maji au chini ya mti ni
kujitafutia majanga mengine, hivyo ni vyema kila mkazi wa mkoa huo akachukua
tahadhari mapema.
No comments:
Post a Comment