Na Mwandishi wetu,
Songea.
WATU nane
wamekutwa wakiwa wamekufa na wengine 25 wakiwa hai katika eneo la makaburi ya
kijiji cha Amani Makolo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambao inadaiwa kwamba
walikuwa wakitoka nchini Ethiopia kwenda Afrika kusini kutafuta maisha.
Inadaiwa kuwa
watu hao ni wahamiaji haramu ambapo walitelekezwa kwenye eneo hilo la makaburi,
huku wakiwa na hali mbaya kutokana na kukosa chakula kwa muda mrefu hali ambayo
ilisababisha wengine kufariki dunia.
Mmoja wa
mashuhuda ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe
aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilibainishwa na wachimbaji
wadogo wa madini aina ya Salphire waliopo katika kijiji hicho, ambao walisikia
sauti za watu wakiongea kutoka eneo hilo la makaburi na ndipo walipofuatilia
waliona kundi la watu hao wakiwa wamelala chini.
Alisema kuwa
baadaye wachimbaji hao waliamua kwenda kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya
kijiji cha Amani Makolo ambao nao walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wilayani
Mbinga na kwamba baadaye walipokwenda katika eneo la tukio wakiwa wameongozana
na mganga kutoka hospitali ya wilaya hiyo ndipo waligundua kuwa watu nane
walikuwa wamekwisha fariki dunia na wengine wakiwa hai huku hali zao zikiwa
taabani.
Alifafanua kuwa
wachimbaji hao wadogo wa madini kwa kushirikiana na wanakijiji waliamua kuchangishana
fedha na kuwanunulia chakula wahamiaji hao haramu ambao baada ya kupata chakula
walianza kuongea kwa ufasaha kwamba walitokea Ethiopia ambapo waliingilia mpaka
wa Namanga mkoani Arusha huku wakiwa wamepakiwa kwenye gari kubwa aina ya Lori
na wao wakiwa wamepakiwa ndani ya kontena.
Kwa upande wake
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Dismas Kisusi alipohojiwa na waandishi
wa habari kuhusiana na tukio hilo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo
alidai kuwa lilitokea Mei 14 mwaka huu majira ya usiku huko kwenye eneo la
makaburi hayo ya kijiji cha Amani Makolo.
Kisusi alifafanua
kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa wamebebwa kwenye Lori hilo ambalo
lilikuwa na kontena ambamo ndimo walihifadhiwa wahamiaji hao ambao walikuwa
wakisafiri kwenda Afrika kusini kupitia ziwa Nyasa.
Aliwataja wahamiaji
haramu nane waliofariki dunia kuwa ni Alado (19), Abeneth (20), Tashara Lile (18),
Ammanuely Abana (20), Degu Abame (18), Manush Abama(19), Moconima Abama(17) na
Gitacho Tamasger (19) ambao wote ni wanaume na kwamba wahamiaji wengine 25 wako
hai na hali zao bado ni mbaya.
Kamanda huyo
alisema kuwa uchunguzi utakapokamilika wahamiaji hao haramu watafikishwa Mahakamani
kujibu mashtaka ya kuingia nchini bila kibali na kwamba aliwaasa wananchi
kujenga tabia ya kutoa taarifa kwa jeshi hilo pindi wanapobaini kuwepo kwa watu
wanaojihusisha na vitendo viovu ikiwemo uvamizi na watu wanaosafirisha
wahamiaji haramu.
No comments:
Post a Comment