Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI wa
shule ya sekondari Kigonsera iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameilalamikia
serikali kwa kutoifanyia ukarabati shule hiyo kwa muda mrefu kutokana na
majengo yake kuwa chakavu jambo ambalo linahatarisha hata usalama wao.
Aidha walisema
kuwa majengo mengi yakiwemo mabweni ya kulala wanafunzi hao, vyumba vya madarasa
ya kusomea pamoja na vyoo yapo katika hali mbaya na kwamba kuna kila sababu sasa
kwa serikali kuchukua hatua juu ya namna ya kuyafanyia ukarabati ili waweze
kuondokana na adha hiyo.
Malalamiko hayo yalitolewa
na wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti,
katika mahafali yao ya 18 ya wahitimu kidato cha sita yaliyofanyika kwenye
viwanja vya shule hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani hapa.
Salum Hassan ambaye
ni mwanafunzi anayetarajia kuhitimu mwaka huu alisema kuwa katika kipindi chote
cha miaka miwili ambayo yeye na wenzake wameishi shuleni hapo, wamekuwa
wakikumbana na adha hiyo huku wakati mwingine wakihofia hata kuangukiwa na
majengo ya shule hayo kutokana na uchakavu uliopo.
“Majengo haya
tokea yajengwe miaka ya sitini hayajafanyiwa ukarabati viongozi wengi wamekuwa
wakitembelea shuleni hapa na kujionea namna majengo yalivyochakaa lakini hakuna
hatua tunayoweza kuiona ya kufanyiwa ukarabati mkubwa kwa kweli inasikitisha
sana”, alisema Hassan.
Emmanuel Sanga, David
Mhande na Vamentine Wella nao walieleza kuwa wakati umefika sasa kwa wale viongozi
wenye dhamana ya kusimamia masuala ya elimu hapa nchini, wahakikishe wanaiangalia
shule ya sekondari Kigonsera kwa jicho la huruma kwani shule hiyo ni kongwe na ambayo
viongozi wengi wamesoma hapo akiwemo Rais mstaafu Benjamini Mkapa na Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, kwa kuhakikisha inafanyiwa ukarabati huo ili iweze kuendelea
kudumu miaka mingi ijayo kwa faida hata ya kizazi cha sasa na baadaye.
Walifafanua kuwa
endapo kama hakuna hatua zitakazoweza kuchukuliwa kwa haraka katika kunusuru
hali hiyo kuna uwezekano mkubwa ukafika wakati shule hiyo ikafungwa na watoto
wakarudishwa majumbani kwao kutokana na uchakavu huo wa majengo.
“Hali ya shule
yetu siyo nzuri kabisa ni vyema serikali ikaipatia kipaumbele kwa kuifanyia
ukarabati wa hali ya juu ili kudumisha usalama wa wanafunzi wanaosoma hapa shuleni”,
walisema.
Awali Kaimu Mkuu
wa shule hiyo, Jema Yohana katika taarifa yake alimweleza mgeni rasmi wa
mahafali hayo ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kuwa shule ya
sekondari Kigonsera yenye kidato cha tano na sita ina jumla ya wanafunzi 850
ambapo wanafunzi wa kidato cha sita ni 432 na kidato cha tano ni 418 na kwamba
imekuwa ikiendelea kufanya vizuri katika nyanja ya taaluma kwa kupiga hatua mbele
kila mwaka na kujiwekea mkakati wa kufuta daraja sifuri.
Jema alibainisha
kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa ni kihunzi
katika kufikia malengo yaliyowekwa ambapo alizitaja changamoto hizo kuwa ni
uchakavu huo wa miundombinu ya majengo, upungufu wa nyumba za watumishi, ubovu
wa barabara iingiayo kwenda shuleni pamoja na daraja, uchakavu wa magari na
ukosefu wa baadhi ya watumishi wa kada mbalimbali.
Kwa upande wake
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alisema kuwa changamoto zinazoikabili shule
hiyo zitafanyiwa kazi na serikali na kuwataka wataalamu wa majengo kwenda
shuleni hapo kuangalia namna miundombinu ilivyochakaa ili hatimaye gharama
halisi ya ukarabati iweze kufahamika na hatua zichukuliwe.
Pia Nshenye
aliwaasa wahitimu wa kidato cha sita kwa kipindi watakachokuwepo majumbani kwao
wasijiingize na makundi maovu ambapo kwa kufanya hivyo kutakuwa na uwezekano
mkubwa wa kufuta ndoto zao za kujiendeleza kimasomo.
Pamoja na mambo
mengine alisisitiza kuwa hivi sasa wanapaswa kushiriki katika shughuli za
kimaendeleo na sio kupoteza muda mwingi kukaa vijiweni bila kazi muhimu ya
kufanya na kwamba, inafaa pia wafahamu duniani kote kuna tatizo la ukosefu wa
ajira hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo wahakikishe kwa wale ambao
watapata fursa ya kujiunga hata kwenye vyuo vya ufundi wasipuuze kwani ni moja
kati ya sekta ambayo imekuwa ikiwafundisha vijana fani mbalimbali ambazo ni
rahisi kujiajiri.
No comments:
Post a Comment