Na Kassian
Nyandindi,
Mbeya.
WAANDISHI wa habari Nyanda za juu kusini ambao wameshiriki
kwenye mafunzo ya namna ya kuandika habari za manunuzi ya umma, wametakiwa huko
waendako wakafanye kazi kwa weledi na kuleta mabadiliko chanya kwa manufaa ya jamii
na taifa kwa ujumla.
Aidha imeelezwa kuwa wanapaswa kazi zao kuzifanyia uchunguzi
wa kina kabla ya kuujulisha umma ili ziweze kuleta tija na kwamba kipengele cha
habari za manunuzi kimekuwa na ombwe kubwa ambalo linahitaji kuzibwa kwa kuandika
habari hizo kwa uwazi na ukweli.
Hayo yalisemwa na Monica Malikita ambaye ni Mkufunzi wa
mafunzo ya uandishi wa habari za manunuzi ya umma (PPRA) kutoka Kanda ya
Dodoma, ambayo yaliwakutanisha waandishi hao kwa siku tatu na kufanyika kwenye ukumbi
wa Mkapa Jijijini Mbeya.
“Tunataka kuona huko muendako mnakwenda kuripoti habari za
manunuzi kwa weledi na mnaendelea kuujulisha umma kinagaubaga kwa kila jambo
litakalokuwa linatokea katika vipengele vya manunuzi ya umma, hasa kwenye
halmashauri za wilaya ambako ndiko shughuli za manunuzi zimekuwa zikifanyika
mara kwa mara”, alisema Malikita.
Naye Castor Komba ambaye ni Mkufunzi wa mafunzo hayo
aliongeza kuwa lengo la mada walizofundishwa waandishi hao ni kuwafanya pia
waweze kuelewa sheria za manunuzi hayo na marekebisho yake, ikiwemo masuala ya
usimamizi wa mikataba na uhalisia wa thamani ya fedha iliyotumika kwenye mradi
husika.
Komba aliongeza kuwa sheria mama ya manunuzi ya umma ya mwaka
2011 baadhi ya vipengele vimekuwa vikisisitiza na kutoa maelekezo kwa watendaji
husika katika taasisi za umma kufanya kazi kwa kufuata misingi na taratibu
zilizowekwa na sio vinginevyo.
Alifafanua kuwa kwa upande wa halmashauri za wilaya, siku
zote msimamizi Mkuu wa manunuzi ya umma ni Mkaguzi wa ndani (Internal Auditor)
hivyo kazi yake kubwa anapaswa kuhakikisha kwamba taratibu za manunuzi
zinazingatiwa wakati wote bila kufanyika au kuwepo kwa ukiukwaji wa aina yoyote
ile.
Hata hivyo naye Henry Muhanika ambaye ni Mjumbe wa Baraza la
Habari Tanzania (MCT) alisisitiza pia umefika wakati sasa kwa wanahabari wote
Tanzania, kuondoa hofu na uoga katika utendaji wa kazi zao za kila siku hasa
pale wanapofikia hatua ya kuibua mambo ambayo yanalenga kuinufaisha jamii kwa
manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment