Sunday, April 23, 2017

MAOFISA UGANI WAZEMBE MKOANI RUVUMA WATAFUTIWA MWAROBAINI WAO

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amesema kwamba Maofisa ugani waliopo katika mkoa huo wengi wao wamekuwa wakifanyabiashara zao binafsi, badala ya kutekeleza majukumu ambayo wamepewa na serikali katika kuwatumikia wananchi vijijini kwenye shughuli za kilimo.

Aidha amewanyoshea kidole akieleza kuwa serikali itawachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya hivyo, ikiwemo kufukuzwa kazi ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

DKt. Mahenge alisema hayo juzi alipokuwa akihutubia kwenye kikao cha Wadau wa kahawa Kanda ya Ruvuma, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hanga uliopo katika Manispaa ya Songea mjini hapa.

Alisema kuwa wataalamu hao wa masuala ya kilimo wanapaswa kwenda vijijini kuwatumikia wakulima kwa kuhakikisha wanawapatia mbinu bora za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili yaweze kuwa yenye ubora unaokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.


Alieleza kuwa malalamiko yamekuwa yakitolewa kutoka kwa baadhi ya wakulima mkoani humo kwamba, maofisa wengi wa kilimo wakiwemo pia maofisa ushirika wamekuwa ndio chanzo cha kudumaza maendeleo katika sekta ya kilimo mkoani hapa, kwa kile alichodai kuwa muda mwingi wamekuwa wakionekana maeneo ya mjini wakifanya shughuli zao binafsi badala ya kutekeleza majukumu waliyopewa na serikali.

Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge alisema kuwa hata hali ya uzalishaji wa zao la kahawa mkoani humo maendeleo yake yamekuwa yakisuasua hivyo kuna kila sababu sasa kwa viongozi waliopewa dhamana kuchukua hatua ya kuhakikisha kwamba, mkulima anaelimishwa ipasavyo namna ya kutumia mbinu bora za uzalishaji wa zao hilo ikiwemo matumizi bora ya pembejeo ambayo huongeza uzalishaji wakati wa msimu wa mavuno.

“Utakuta maofisa kilimo wa hapa kwetu Ruvuma wengi wao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea, wanafanya biashara zao binafsi badala ya kutekeleza majukumu waliyopewa na serikali natoa agizo kwa halmashauri zote ndani ya mkoa wangu, juhudi za dhati ziwekezwe kwa kumsimamia mkulima azalishe mazao bora ambayo yameandaliwa katika mazingira mazuri”, alisisitiza Dkt. Mahenge.

Vilevile katika msimu wa mwaka 2015/2016 mkoa huo ulizalisha tani 17,519 za kahawa na kufikia hatua ya kushuka uzalishaji huo kwa kuzalisha tani 13,733 msimu wa 2016/2017 ambapo kushuka huko ni sawa na wastani wa asilimia 21 ya uzalishaji wa zao hilo.


Hata hivyo mkoa wa Ruvuma hivi sasa una kazi kubwa iliyopo mbele yao kwa viongozi husika kuhakikisha kwamba uzalishaji wa zao la Kahawa unaongezeka katika msimu wa mwaka 2017/2018 baada ya kujiwekea mikakati kwamba uzalishaji katika msimu huo unapaswa kufikia tani 18,000.

No comments: