Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye ametoa
amri ya kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaokiuka amri halali
ya kupambana na ugonjwa wa homa ya nguruwe, African Swine Fever ambao umeingia katika
halmashauri ya wilaya hiyo.
Cosmas Nshenye. |
Nshenye ametoa amri hiyo kupitia nakala yake ya barua ya
Aprili 10 mwaka huu yenye kumbukumbu namba AB. 120/475/01/18 iliyosambazwa kwa viongozi
wa wilaya hiyo ambayo mwandishi wetu anayo nakala yake ikisisitiza juu ya namna
ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Mimi Mkuu wa wilaya hii kwa mujibu wa sheria ya
Veterinari ya mwaka 2003 na sheria ya magonjwa ya mifugo natoa amri ya
kuwachukulia hatua wale wote watakaoshindwa kufuata maelekezo, amri, zuio na
katazo hili ambalo limetolewa kisheria chini ya mamlaka halali ya sheria
kifungu cha 62 – 1 cha masharti ya karantini dhidi ya ugonjwa wa homa ya
nguruwe”, alisema Nshenye.
Alisema kuwa amri hiyo ni pamoja na kuzuia kutoa au
kuingiza nguruwe pamoja na mazao yake kama vile nyama na mbolea katika
halmashauri ya wilaya ya Mbinga bila idhini ya Daktari wa mifugo
aliyeidhinishwa.
Pia alieleza kuwa wanapaswa wafugaji wote kuanza sasa
kunyunyiza dawa katika maeneo yote ya ufugaji ambao mabanda yao yamepata
ugonjwa huo, ili kuweza kuangamiza vimelea vya ugonjwa na wafugaji wajenge
mabanda hayo vizuri ili kuzuia kuzurula wanyama hao hovyo mitaani.
Kwa upande wake naye Daktari wa mifugo wa halmashauri ya
wilaya ya Mbinga, Dkt. Patrick Banzi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa
ugonjwa wa African Swine Fever huenea kwa kulisha nguruwe masalia ya nyama ya
nguruwe mwenye ugonjwa, maji, majani, chakula, na mtu ambaye amevaa buti ambazo
zimekanyaga kutoka eneo la mabanda ambayo yana ugonjwa.
Vilevile nguruwe mwenye homa kugusana na nguruwe ambaye
hana ugonjwa na pia husambazwa na wadudu warukao au wang’atao kama vile kupe.
Kadhalika alifafanua pia dalili za ugonjwa huo kwa
mnyama huyo kuwa ni pamoja na nguruwe
wagonjwa kujitenga na wenzao, kunyongeka, kukosa hamu ya kula, kupenda kukaa
muda mwingi kwenye kivuli, kujikusanya pamoja, kuhema kwa shida na kwa wale
wenye ngozi nyeupe ngozi yao kuwa nyekundu hasa maeneo ya chini na miguu.
Dkt. Banzi alieleza dalili zingine kuwa ni wengine huwa
wanaharisha damu, hupata mafua au kutoa mate yenye povu povu ambayo huwa na
damu na kutapika, miguu ya nyuma kukosa nguvu na kuwa dhaifu na hukaa kama
mbwa.
No comments:
Post a Comment