Na Kassian
Nyandindi,
Namtumbo.
KATIKA kuhakikisha kwamba huduma za tiba zinaendelea
kuboreshwa, wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imejiwekea mikakati ya kuhamasisha
wadau mbalimbali kuchangia ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo, ili ujenzi huo
uweze kufanyika kwa urahisi.
Luckness Amlima. |
Aidha kampeni ya uhamasishaji huo itafanyika kuanzia mwezi
Julai mwaka huu na kwamba fedha zitakazopatikana, zitaweza kufanya kazi ya
ujenzi wa majengo ya hospitali pamoja na kuimarisha miundombinu mingine katika
sekta ya afya wakati ujenzi huo utakapofanyika.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Luckness Amlima alisema hayo jana
alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi juu ya mikakati yake ya kukuza
maendeleo katika sekta hiyo ya afya wilayani humo.
Amlima alisema kuwa wananchi waliopo ndani ya wilaya hiyo na
nje ya wilaya anawaomba wajitokeze kwa wingi wakati kampeni hiyo
itakapozinduliwa ili kuweza kufikia malengo ambayo wilaya imejiwekea katika
kupambana na kufikia malengo ya ujenzi wa hospitali hiyo.
“Wilaya hii tokea ianzishwe hatuna hospitali hivyo kuna kila
sababu sasa kwa sisi viongozi kuwa wabunifu katika kukabiliana na tatizo hili kwa
vitendo ili katika sekta hii ya afya endapo tunafanikiwa kujenga hospitali yetu
tuweze kuokoa vizazi vyetu”, alisema Amlima.
Vilevile akizungumzia kwa upande wa vituo vya afya na
zahanati vilivyopo huko vijijini, alisisitiza kuwa serikali pia itaendelea
kuboresha huduma husika hivyo anawaomba wananchi kuendelea kujitolea katika ujenzi
wa majengo na miundombinu mingine mbalimbali ili kuweza kufikia malengo hayo.
Hata hivyo alisisitiza juu ya suala la wananchi kujitokeza
kwa wingi na kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo kampeni hiyo
itakapoanzishwa ndani ya wilaya ya Namtumbo, itakuwa inafahamika kwa jina la
‘Afya Kwanza’ na kwamba wadau wote watapewa taarifa ili waweze kushiriki
kikamilifu kwenye kampeni hiyo.
No comments:
Post a Comment