Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KATIKA kuhakikisha kwamba mazingira yanaendelea kuboreshwa
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, idara ya kilimo katika Manispaa hiyo imegawa
bure miche bora ya matunda kwa watumishi wake wa idara mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisa habari wa
Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa uongozi wa Manispaa umefanya hivyo
kwa lengo la kuwajenga watumishi wake, kuwa na tabia ya mara kwa mara kupenda
kupanda miti ya matunda na miti mingine ya aina mbalimbali ili kusaidia kuhifadhi
mazingira na watu kuweza kupata matunda.
Midelo alifafanua kuwa Manispaa ya Songea, imenunua miche
bora ya matunda 2000 yenye thamani ya shilingi milioni 5,000,000 kutoka Chuo Kikuu
cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA).
Kwa upande wake Ofisa kilimo wa Manispaa hiyo, Zawadi Nguaro naye
alieleza kuwa miche yote iliyonunuliwa ni ya matunda kati ya hiyo kuna miche
aina tano za maembe na miche aina mbili za mapalachichi.
“Lengo letu la idara ni kuhakikisha watumishi wetu wanakuwa
na utamaduni wa kupanda miti na kuitunza kila mwaka, ili kuhifadhi mazingira na
kupata matunda bora ambayo ni muhimu kwa afya na kuwaongezea kipato”, alisema
Nguaro.
Miongoni mwa watumishi waliofaidika na miche hiyo ni Katibu
tawala wa wilaya ya Songea Pendo Ndumbaro na Madiwani wa Manispaa hiyo.
Pia Nguaro aliwaasa watumishi hao ambao walipewa miche hiyo
kuhakikisha kwamba wanaitunza vizuri, ili iweze kukua na kuanza kuzaa matunda
ambayo itakuwa ni faida kwa kizazi cha sasa na kijacho.
No comments:
Post a Comment