Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma wametuma ujumbe wa wafanyabiashara wenzao watano na wazee watano kwenda
Dodoma kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa lengo la kupeleka kilio chao baada
ya Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema kudaiwa kuwafungia vibanda vyao vya
biashara, tangu Februari 11 mwaka huu kwa madai kwamba wanadaiwa shilingi
milioni 100 na halmashauri hiyo jambo ambalo wamekana na kueleza kuwa sio la
kweli.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Masoko katika Manispaa ya
Songea (UWABIMASO) Leonard Chiunga alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza
kwenye mkutano wa dharura na wafanyabiashara hao, uliofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Chama cha walimu Songea uliopo mjini hapa ambao ulihudhuriwa pia na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania mkoa wa Ruvuma, Issaya
Mwilamba.
Chiunga alisema kuwa tokea maduka hayo yalipofungwa wateja
ambao wamekuwa wakienda kwa ajili ya kupata mahitaji kwenye maduka hayo wanashindwa
kupata mahitaji husika, jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kwao hivyo wanaziomba
mamlaka za juu zione umuhimu wa kuchukua hatua haraka kuyafungua ili hata
wafanyabiashara hao nao wasiweze kupata hasara kutokana na kuyafunga huko.
Alifafanua kuwa Mkuu wa wilaya, Mgema akiwa ameongozana na Kamati
yake ya ulinzi na usalama majira ya saa tatu asubuhi ndiyo aliweza kuchukua jukumu
la kuyafunga maduka hayo ambayo ni 275 yaliyopo kwenye vibanda vya Soko kuu lililopo
mjini hapa, kwa madai kuwa wafanyabiashara wanatakiwa waingie mikataba upya na
halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa lazima na pango la vibanda hivyo inabidi
lipande kwa asilimia mia moja jambo ambalo alidai kuwa ni kinyume na makubaliano
ya vikao mbalimbali vilivyofanyika.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa mnamo Januari 27 mwaka huu
kilifanyika kikao katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ambako waliazimia kuwa
halmashauri ya Manispaa hiyo ni lazima ijiridhishe kwa kukaa pamoja na
wafanyabiashara hao na kujadili jambo hilo kabla haijachukua maamuzi magumu
kama hayo bila kuwashirikisha walengwa.
Alisema kwamba wafanyabiashara wameshangazwa kuona Mkuu wa
wilaya hiyo, Mgema kuchukua uamuzi wa kufunga vibanda hivyo vya wafanyabiashara
kwa kutumia nguvu wakati jambo hilo bado lipo kwenye vikao vya mazungumzo na
kwamba Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge aliahidi kuumaliza mgogoro
huo.
Kadhalika alieleza kuwa kufuatia kuendelea kufukuta kwa
mgogoro huo viongozi wa wafanyabiashara hao wameunda Kamati ya usuluhishi
ambayo ina Wajumbe kumi, wakiwemo wazee watano wa halmashauri ya Manispaa ya
Songea ambao wameondoka Februari 12 mwaka huu majira ya asubuhi kwenda Dodoma
kumuona Waziri Mkuu, Majaliwa ili aweze kuwasaidia kumaliza tatizo hilo ambalo
linaonekana viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuwakandamiza wafanyabiashara hao
wakitaka wasaini mikataba ambayo sio rafiki kwao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara
Tanzania (JWT) mkoani Ruvuma, Issaya Mwilamba alisema kuwa kitendo cha uongozi
wa wilaya ya Songea kwa kushirikisha na Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya
hiyo kwenda kufunga vibanda hivyo kwa kutumia nguvu ni kosa hivyo wanaiomba
serikali iingilie kati ili waweze kumaliza mgogoro huo.
Mwilamba alisema kuwa kwa muda mrefu sasa halmashauri ya Manispaa
ya Songea imekuwa na migogoro mingi isiyokuwa na mwisho ambayo imekuwa
ikiendekezwa kwa kufuata majungu jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya
wananchi na taifa kwa ujumla.
Vilevile Mkuu wa wilaya ya Songea, Mgema alipoulizwa na
mwandishi wa habari hizi kuhusiana na mgogoro huo alithibitisha kuvifunga
vibanda vya maduka hayo vinavyozunguka Soko kuu mjini hapa, huku akiongeza kuwa
bado anafanya kwanza mazungumzo na wahusika ili aweze kumaliza tatizo hilo.
Mkuu wa mkoa Ruvuma Dkt. Mahenge naye alikiri kuwepo kwa hali
hiyo na kueleza kuwa tayari alikwisha anza kuufanyia kazi mgogoro huo na kwamba
hivi sasa yupo Dodoma kikazi, ambapo atakaporudi atahakikisha jambo hilo
linakwisha.
No comments:
Post a Comment