Waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto, Ummy Mwalimu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANAFUNZI wanaosoma katika chuo cha Maafisa tabibu Manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma, wameilalamikia serikali kwa kitendo cha kusitisha
huduma ya kutoa chakula chuoni hapo jambo ambalo linawafanya baadhi yao
kushindwa kumudu gharama za kununua chakula hicho na kuwafanya waishi maisha
magumu.
Aidha kufuatia hali hiyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa
habari hizi umebaini pia wanafunzi wa kike, baada ya muda wa masomo hujiuza
kimwili mitaani kwa kufanya mapenzi ili waweze kupata fedha za kujikimu ikiwemo
kununua chakula na kuendesha maisha yao.
Kadhalika wanafunzi hao wapo hatarini kuambukizwa na magonjwa
kutokana na mazingira ya chuo hicho, ikiwemo vyoo na mabafu ya kuogea wanafunzi
kuwa katika hali mbaya.
Vilevile majengo yanayotumika kulala wanafunzi hao nayo
yamekuwa chakavu kutokana na serikali, kutoyafanyia ukarabati kwa miaka mingi
na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa miundombinu ya chuo hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi mjini
hapa, wanafunzi hao walisema kuwa chuoni hapo miaka miwili iliyopita serikali
ilikuwa ikisambaza chakula kupitia wazabuni, lakini huduma hiyo imesitishwa
ghafla na sasa wanalazimika kuchangishana fedha kila mwezi ili waweze kupata
chakula.
“Kwa upande wa huduma ya umeme na maji tumekuwa pia
tukichangishana fedha kulipia gharama husika ili tuweze kuishi na kuendesha
masomo hapa chuoni, tunaiomba serikali itatue matatizo haya tuliyonayo kwani
yanatufanya tuwe katika hali ngumu kimaisha”, walisema.
Akihojiwa na mwandishi wetu ofisini kwake, Mkuu wa chuo hicho
Dkt. Salustian Salla alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa majengo
ya chuo hicho cha maafisa tabibu tangu yajengwe mwaka 1974, yamefanyiwa
ukarabati mara moja tu kipindi cha utawala wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu
Benjamin Mkapa.
Dkt. Salla alisema kuwa chuo hicho ambacho kinamilikiwa na
Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanafahamu juu ya
changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo uchakavu wa majengo hayo.
“Hili la wanafunzi kujiuza kwa kweli sijawahi kusikia, lakini
tumekuwa na changamoto nyingi miundombinu yetu haifai kwa matumizi ya binadamu
hivyo wakati mwingine tumekuwa tukilazimika kutumia ada za wanafunzi kukarabati
vyoo ambavyo sakafu zake hubomoka”, alisema Dkt. Salla.
Aliongeza kuwa changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni
ukosefu wa walimu wa kufundisha darasani ambapo mpaka sasa, chuo kina walimu
wawili tu na kwamba wakati mwingine hulazimika kuomba madaktari wanaotoka nje
ya chuo hicho kwa ajili ya kufundisha wanafunzi hao.
Pamoja na mambo mengine, akizungumzia juu ya huduma ya
chakula chuoni hapo alifafanua kuwa katika kipindi cha nyuma serikali ilikuwa
inaleta fedha kwa ajili ya kununua chakula cha wanafunzi na kwamba
wamesimamisha kutoa huduma hiyo kutokana na sababu ya kushindwa kulipa
wazabuni.
“Kama unavyoona mazingira ya chuo chetu, hatuna hata uzio
kuzunguka chuo hiki watu wamekuwa wakiingia katika maeneo ya chuo bila kufuata
utaratibu kwani hata usalama wa mazingira yetu ni mdogo”, alisema.
Hata hivyo alisema ni miaka miwili sasa imepita tokea serikali
isitishe huduma ya wazabuni kusambaza chakula kwa wanafunzi wa chuo cha maafisa
tabibu katika Manispaa ya Songea na mpaka sasa bado hawajalipwa fedha zao kwa
kazi waliyofanya ya kusambaza chakula hicho.
No comments:
Post a Comment